Jun 23, 2016 22:46 UTC
  • Ijumaa 24 Juni 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Ramadhani 1437 Hijria sawa na tarehe 24 Juni 2016.

Tarehe 24 Juni miaka 204 iliyopita, Caracas mji mkuu wa Venezuela ulidhibitiwa na Simon Bolivar ikiwa ni wakati wa mapambano ya mpigania uhuru huyo dhidi ya wakoloni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya Amerika ya Kusini. Mkoloni Muhispania alishindwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja na baada ya ushindi huo Simon Bolivar anayejulikana kama shujaa wa mapambano dhidi ya wakoloni huko Amerika Kusini, aliasisi Shirikisho la Colombia Kubwa. Shirikisho hilo lilijumuisha nchi za Venezuela, Colombia, Panama na Ecuador, na Bolivar alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo.

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsia, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran.

Na tarehe 4 Khordad miaka 53 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alihamishiwa katika kambi ya kijeshi ya Ushratabad baada ya kukamatwa na Shirika la Usalama la Shah maarufu kwa jina la Savak. Siku 40 baada ya kushikiliwa katika kambi hiyo, Imam Khomeini kwanza alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq. Katika kipindi chote cha miaka 13 ya kubaidishiwa nje ya nchi, Imam aliongoza harakati zake za mapinduzi kupitia wanafunzi wake waliokuwa wakiwasilisha ujumbe zake kwa wananchi ndani ya Iran. Februari mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini na kupokewa na watu milioni tano. Siku 10 baadaye Imam alifanikiwa kuuangusha utawala wa kifalme ulioiongoza Iran kwa kipindi cha miaka 2500.