Jun 28, 2023 02:20 UTC
  • Jumatano, tarehe 28 Juni mwaka 2023

Leo ni Jumatano tarehe 9 Dhulhija 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 Juni mwaka 2023.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhilhaji. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa, na Hadithi nyingine za Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa, Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahali pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija. 

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi huko Kufa nchini Iraq.

Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa eneo hilo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua mjukuu huyo wa Mtume wakimtaka aende Kufa na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya.

Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa, na wakamuacha Muslim bin Aqil peke yake.

Haram ya Muslim bin Aqil, Kufa

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, Kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake.

Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza ujenzi huo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini.

Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Ratiba na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika kituo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyowavutia sana Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika eneo hilo muhimu. Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kupatwa na wahka na hivyo kutafuta kisingizio cha kusitisha au hata kufunga kabisa shughuli zake. 

Kituo cha Kiislamu cha Washington

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Ruhullah Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu.

Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi wengine 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa. 

 Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti 

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq.

Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein.

Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake.

Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran. 

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza.

Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja.

Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina inliyokuwa ikiongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi". Mbali na hayo, mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.   

Gaza

 

Tags