Jumapili, Juni 26 2016
Leo ni Jumapili tarehe 20 Ramadhan mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 26 Juni 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita na kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya historia, jeshi la Kiislamu chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makkah. Uvunjwaji wa makubaliano ya amani ya Hudaibiyyah uliofanywa na makafiri wa Kikuraish hapo mwaka wa nane Hijiria, makubaliano ambayo awali yalitiwa saini baina ya mtukufu Mtume (saw) na viongozi wa makabila ya Kikuraish, ulipelekea jeshi la Kiislamu lenye wapiganaji elfu 10 kwa uongozi wa Mtume kuweza kuukomboa mji huo muhimu. Hii ni katika hali ambayo katika kukombolewa mji huo, Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha wa jumla kwa makafiri wa Makkah ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiendesha mapambano makubwa ya kuzuia kuenea kwa dini ya Uislamu sanjari na kumfanyia maudhi makubwa Mtume huyo wa Allah na wafuasi wake. Kitendo hicho cha huruma kilichofanywa na Nabii Muhammad kiliwafanya watu wa makabila mengi ya Kikuraish kuingia kwenye dini hii. Ni kwa ajili hiyo ndio maana ukombozi wa mji wa Makkah ukajiri bila ya mapigano wala umwagaji damu wowote.
Siku kama ya leo miaka 895 iliyopita, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, mtaalamu wa fasihi na nahawu wa Kiislamu. Ibn Shajari aliyefahamika pia kwa jina la Abu al-Saadat Hibatullah Bin Ali Alawi Hassani, malenga, wa Kishia na mtaalamu wa lugha na nahawu, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya Ibn Shajari inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) na ni kwa ajili hiyo ndio maana akapewa lakabu ya ‘Alawi.’ Akiwa kijana mdogo alianza kujifunza elimu ya fasihi, nahawu, hadithi na elimu nyingine mashuhuri za wakati wake na daima alilipa umuhimu mkubwa suala la kusoma jambo ambalo lilimfanya kufikia daraja kubwa za kielimu akiwa kijana mdogo. Kwa kipindi cha miaka 70, Ibn Shajari Baghdadi alijishughulisha na ufundishaji wa elimu ya nahawu ambapo idadi kubwa ya watu walipata kusoma kwake elimu hiyo.
Siku kama ya leo miaka 811 iliyopita alifariki dunia Ibn Yaqut Himawi, mtaalamu mashuhuri wa Kiislamu wa elimu ya jiografia. Abdullah Yaqut Bin Abdullah Rumi, maarufu kwa jina la Yaqut Himawi na ambaye ni miongoni mwa wataalamu wa elimu ya fasihi wa karne ya saba Hijiria, alizaliwa mwaka 539 Hijiria mjini Baghdad Iraq. Alifanya safari nyingi na kutalii na kufikia daraja ya juu katika ulingo wa elimu ya jiografia. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyo ni pamoja na vitabu vya ‘Muujamul-Buldan’ na ‘Muujamul-Udabaa.’
Siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini, na alikuwa akisoma mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga pia nyimbo za hamasa na za kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, sawa na tarehe 26 Juni 1945 Miladia, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko nchini Marekani kwa kupasishwa makubaliano ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki wa vita hivyo.
Na siku kama ya leo miaka 56 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa, ambapo siku hii kila mwaka husherehekewa nchini humo kama siku ya taifa. Kuanzia katikati mwa karne ya 18 Miladia, Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani baina yazo kwa lengo la kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika. Sababu hiyo ilipelekea kudhibitiwa mara kadhaa kisiwa hicho na nchi mbili hizo na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19 Miladia, Ufaransa ikafanikiwa kukidhibiti kikamilifu kisiwa hicho. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.