Usikichome, Leta Mfano Wake Kama Unaweza!
(last modified Thu, 17 Aug 2023 07:13:42 GMT )
Aug 17, 2023 07:13 UTC
  • Usikichome, Leta Mfano Wake Kama Unaweza!

Siku moja miaka mingi sana iliyopita, yaani miaka elfu mbili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as), watu wa Namrud (Nimrodi) walikuwa wamerejea makwao kutoka kwenye shughuli ya kidini.

Siku hiyo kulitukia jambo la ajabu! Waliyakuta masanamu waliyokuwa wakiyaabudu yakiwa yamevunjwa na kuanguka chini... 

 Walijiuliza: Nani ameifanya hivi miungu yetu?!

Baadhi yao walijibu: “Tulimsikia kijana mmoja akiwazungumzia vibaya; Jina lake ni Ibrahim... Alikuwa akisema: "Kwa nini mnaabudu viumbe ambavyo havina faida yoyote kwenu badala ya Mwenyezi Mungu? Kefle kwenu na hivyo mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Hivi kwa nini hamtii akilini?"

Waliendelea kusimulia kwamba: Inaonekana Ibrahimu alivunja masanamu haya na kutundika shoka kwenye shingo ya sanamu kubwa wakati tulipokuwa nje ya mji. Walisema: Mleteni mbele ya macho ya watu wapate kumshuhudia. Kisha walimuuliza: Je, wewe ndiwe uliyeifanyia haya miungu yetu? Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.  (Anbiya 59-67)

Baadhi yao walirejea kwenye nafsi zao na kuanza kufikiria. Walijua kwamba, miungu yao ya masanamu haiwezi kufanya chochote. Namrudi, mtawala dhalimu wa wakati huo katika eneo la Mesopotamia, alibakia bumbuazi na hakuwa na uwezo wa kujibu hoja za Ibrahimu. Kwa upande mwingine, alikuwa akiwaona baadhi ya wafuasi wake wakikubali imani ya Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na kuingia kwenye dini ya Ibrahim; hivyo hakuwa na njia nyingine isipokuwa kumchoma moto Ibrahim kama inavyosimulia Aya ya 68 ya Suratul Anbiyaa kwamba:

قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَکُمْ إِن کُنتُمْ فَاعِلِینَ

Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!!

 Hii, ndiyo hatua na harakati zile zile zinazofanywa na akina Nimrodi wa zama hizi huko katika nchi za Magharibi, yaani kuchoma moto Qur'ani na neno la Mungu, baada ya kushindwa mbele ya hoja za kitabu hicho na kukata tamaa kutokana na wimbi kubwa na linalokwenda kwa kasi la mwelekeo wa watu kwenye dini ya Uislamu... Naam, kuichoma moto Qur'ani, sawa kabisa na Nimrodi alivyoamuru kumchomwa moto Mtume wa Mungu, Ibrahim, baada ya kufilisika kifikra na kushindwa kwa hoja!...

Hata hivyo Mwenyezi Mungu Mkarimu aliuamuru moto akisema:

قُلْنَا یَا نَارُ کُونِی بَرْدًا وَسَلامًا عَلَى إِبْرَاهِیمَ

Tulisema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim! 

Karne kadhaa baadaye, Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, alidhihiri katika mji wa Makka, akiwa na kitabu cha "Qur'ani". Walimtishia mara nyingi na kumwamuru atupilie mbali kitabu hicho; kinyume chake, idadi ya wafuasi wake iliongezeka kila siku. Siku moja, viongozi 40 wa Maquraishi walifanya mkutano huko Daru al Nadwa, palipokuwa mahali pa kukutania wakuu na vinara wa Kiquraishi, na wakaamua kumuua Muhammad. Walikubaliana kwamba, kundi la watu watakaowakilisha makabila yote ya Waarabu, litaishambulia nyumba ya Mtume katika giza la usiku na kumuua kwa pamoja akiwa kitandani mwake. Washambuliaji walihesabu masaa na dakika hadi alfajiri na kushambulia kwa pamoja nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Ghafla, Imam Ali bin Abi Twalib alinyanyuka kutoka kwenye kitanda cha mtukufu huyo na kuwafokea:

Ole wenu! Mnafanya nini?!! Walipigwa na butwaa na kubakia bumbuazi. Waliuliza: Muhammad yuko wapi? Ali bin Abi Twalib alijibu akisema: Kwani mlimkabidhi kwangu ili munidai na kuniuliza mahali aliko? Malaika Jibril alikuwa amempasha habari Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu njama hiyo, na mtukufu huyo akaamrishwa na Mola kuhamia Madina.

Makafiri wa Makka walimfuata Mtume (saw) ambaye alikuwa amejificha katika pango la Thaur. Walifuata nyayo hadi kwenye pango hilo, lakini Mwenyezi Mungu Muumba alikuwa amemwamuru mdudu buibui kuweka tando zake kwenye mlango wa pango hilo lililoonekana kana kwamba hajaingia mtu eneo hilo kwa muda mrefu. Waliondoka zao na kurejea Makka. Baadaye, Mtume alitengeneza ustaarabu na jamii mpya huko Yathrib kwa kutumia kitabu chake, yaani Qur'ani. 

Msikiti wa Madina

Sasa, na kutokana na kasi kubwa ya kusambaa Uislamu na wimbi la wanaadamu wanaoikumbatia dini hiyo na mafundisho yake safi, pazia la uongo limeraruka; hivyo kina Nimrodi wa zama hizi wamechoma moto Qur'ani Tukufu wakitaka kuonyesha kwamba, kwanza, wana uadui na msingi wa Uislamu. Na pili, wanaona kuwa, ufahamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Waislamu wenye mwamko kote duniani kuhusu "Uislamu" unavuruga mfumo wa utawala wa kibeberu. Lakini hawajui au hawataki kujua kwamba, moto wa chuki ambao haukumuunguza Nabii Ibrahimu wala kumuangamiza Mtume Muhammad (saw), hauwezi kuitoa Qur'ani, neno na ufunuo la Mwenyezi Mungu, nje ya medani na uwanja wa dunia.

Naam, Qur'ani Tukufu ni muujiza mkubwa wa Mtume Muhammad (saw). Hata hivyo tunapasa kuuliza, je, muujiza unaweza kuchomwa kwa moto?   

 Fikra na kutafakari ni miongoni mwa mada kuu za ujumbe wa Qur'ani. Kitabu hiki cha mbinguni pamoja na mafundisho yake, kina nafasi maalumu katika akili na fikra za watu, na katika Aya zake nyingi, kinasisitiza sana kutafakari juu ya kile kilichosemwa baada ya kutoa ujumbe wake. Kimsingi, neno sahihi linapaswa kubeba ujumbe wa busara na kuimarisha akili na mawazo ya wanaadamu. Qur'ani, ni chombo cha mawasiliano kati ya moyo wa mwanadamu na ubongo. Ni chombo kinachounganisha uwezo wote wa ubongo na moyo wa mwanadamu na asili ya kila kitu, yaani Mola Muumba wa ulimwengu.

 Qur'ani yenyewe imejiarifisha kuwa ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote. Vilevile imejitambulisha kuwa ni mtoa bishara njema na muonyaji wa wanaadamu. Kitabu hiki kitakatifu kinajitaja kwa sifa safi na nzuri kama vile nuru, inayopambanua baina ya haki na batili na inayoongoza kwenye njia bora zaidi, na kuwaondoa wanadamu kwenye minyororo ya kuwaabudu na kuwa watumwa wa wanaadamu wenzao, kwa kuwaelekeza kwenye Tauhidi na ibada ya Mungu Mmoja, Muweza na Mwingi wa rehma..

إِنَّ هَذَا الْقُرْآنَ یَهْدِی لِلَّتِی هِیَ أَقْوَمُ وَیُبَشِّرُ الْمُؤْمِنِینَ الَّذِینَ یَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا کَبِیرًا

Hakika hii Qur'ani inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa, na inawabashiria waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa. (Israa: 9) 

Qur'ani, imesimulia hadithi na visa vingi vya manabii na mataifa yaliyopita. Lakini kwa kuwa makusudio ya Qur'ani ni kuwaongoza watu, katika hadithi hizo, yanatajwa tu yale yanayohitajika kuwaongoza wanaadamu ili waja wapate kujifunza kutokana na matukio hayo. Ni dhahiri kwamba, ni jambo muhimu na la dharura sana kwa wanaadamu kujifunza na kupata ibra kutokana na matukio ya zama zilizopita kama inavyosema Aya ya 111 ya Suratu Yusuf kwamba: لَقَدْ کَانَ فِی قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِی الأَلْبَابِ

"Kwa hakika katika simulizi zao kuna mazingatio kwa wenye akili.."

Kwa upande mwingine, sharti la kuweza kutoa majibu na kukidhi mahitaji ya mwanaadamu ni kwamba kitabu hiki kisizeeke na kiwe safi na kipya zama na nyakati zote. Kwa msingi huo, maudhui ya Qur'ani Tukufu yamekusanywa kwa namna ambayo, kila mtu, katika zama zote, anaweza kuketi kwenye meza hiyo na kufaidika na baraka zake zisizo na mwisho. Khalifa wa Mtume wetu Muhammad (saw), Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) anasema: 

واعلموا أن هذا القرآن هو الناصح الذی لا یغش، والهادی الذی لا یضل، والمحدث الذی لا یکذب، وما جالس هذا القرآن أحد إلا قام عنه بزیادة أو نقصان: زیادة فی هدى، أو نقصان من عمى.

Na jueni ya kwamba, Qur’ani hii ni mtoaji nasaha isiyoghushi, muongozaji asiyepoteza, na mzungumzaji asiyesema uongo. Haketi mtu yeyote pamoja na Qur’ani hii isipokuwa huinuka hapo akiwa amezidishiwa au kupunguziwa: Ama huzidishiwa uongofu, au hupungukiwa upofu.

 Tangu zilipoteremshwa Aya za kwanza za Qur’ani huko Makka, Muhammad Mwaminifu alisema waziwazi kwamba, Qur’ani si maneno yake binafsi, bali ni neno la Mungu, na kwamba hakuna mwanaadamu anayeweza kuleta mfano wake. Alisema ikiwa hamuamini maneno haya basi, jaribuni kubuni na  kuleta mfano wake kwa kutumia njia zote zinazowekana. Aya ya 203 ya Suratu A'raf inasema: 

وَإِذَا لَمْ تَأْتِهِم بِآیَةٍ قَالُواْ لَوْلاَ اجْتَبَیْتَهَا قُلْ إِنَّمَا أَتَّبِعُ مَا یُوحَى إِلَیَّ مِن رَّبِّی هَذَا بَصَائِرُ مِن رَّبِّکُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ یُؤْمِنُونَ

Na usipowaletea Aya (wakati ufunuo unapochelewa kuteremshwa kutoka kwa Allah) husema: Kwa nini hukuibuni wewe mwenyewe? Sema: Mimi ninafuata yanayofunuliwa kwangu kutokana na Mola wangu. Hii (Qur'ani) ni chombo kinachofungua macho ya (nyoyo) kutoka kwa Mola wenu, na ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini.

 Ujumbe wa Mtume Muhammad (saw), kama Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, ni kuwafundisha watu Kitabu yaani Qur'ani na hekima. Kwa hivyo, alikuwa akifanya haraka kuhifadhi Qur'ani na kujifunza Aya zake, na daima alikuwa na wasiwasi wa neno au hata herufi yake kusahauliwa au kubadilishwa. Wakati huu, Mwenyezi Mungu SW alimtuliza Mtume wake na akamuahidi kwamba, ataihifadhi Qur'ani kifuani mwake na kumrahisishia kusoma na kuelewa maneno na maana yake. Aya ya 9 ya Suratul Hijr inasema: إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّکْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakaoulinda.

Miongoni mwa sifa makhsusi za Qur'ani, ikilinganishwa na vitabu vingine vitakatifu, ni kwamba hakuna yeyote aliyeweza kuchezea na kubadilisha Aya zake, na imebakia kama ilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu bila ya kupotoshwa au kubadilishwa. Kwa hiyo, maneno na sentensi zake ndizo zilezile zilizoteremshwa kutoka kwa Mola Muumba wa dunia na Akhera. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani yenyewe kwamba:

وَإِن کُنتُمْ فِی رَیْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَى عَبْدِنَا فَأْتُواْ بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُواْ شُهَدَاءَکُم مِّن دُونِ اللَّهِ إِنْ کُنتُمْ صَادِقِینَ

Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia mja wetu, basi leteni sura moja mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.

 Na kwa njia hii, Qur’ani inawapa changamoto wakanushaji wote na kuwaita kwenye uwanja wa mapambano na Qur’ani, ili kushindwa kwao katika mpambano huo uwe ushahidi wa wazi wa ukweli wa wahyi na ufunuo huo, na uthibitisho wa usahihi wa utume wa liyekuja nao.

Naam, nasi tunawaambia tena washirikina, majahili na makafiri wa zama hizi, kama ilivyofanya Qur'ani kwa washirikina wa Makka kwamba, msikichome, bali leteni mfano wake, laa… bali leteni hata Aya moja tu mfano wa Aya zake, kama mnaweza!