Quds, Kituo cha Dini za Mwenyezi Mungu-2
Hatua ya Rais Donald Tump wa Marekani ya kuitambua Quds (Baitul Muqaddas au Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel kwa mara nyingine imeuweka mji huo mtakatifu kwa dini zote za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu katika kurasa za mbele za magazeti na safu ya kwanza ya habari za vyombo vya mawasiliano ya umma kote duniani.
Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia nafasi ya Msikiti wa al Aqsa huko Quds (Jerusalem) kwa Waislamu na vilevile Miiraji na safari ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mbinguni na katika ulimwengu wa juu wa malakuti. Aya ya kwanza ya Quratul Israa inasema: Ametakasika (Mwenyezi Mungu) aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Mfasiri mkubwa wa Qur'ani na mwandishi wa tafsiri ya al Miizan, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai anasema: Maana ya "tumevibariki vilivyo kandokando yake" katika aya hii ni kwamba Msikiti wa al Aqsa mbali na kwamba wenyewe ni eneo takatifu, maeneo ya kandokando yake pia ni ardhi iliyobarikiwa. Baraka hizi zinaweza kuwa zile za dhahiri kama ardhi yake yenye rutuba, miti, mito ya maji na mandhari ya kuvutia, na vilevile baraka za kimaanawi na kiroho za Baitul Muqaddas. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ardhi hii takatifu ilikuwa makazi ya Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha historia na kituo cha Tauhidi na ibada ya Mungu Mmoja", mwisho wa kunukuu.
Nukta nyingine iliyomo katika safari hiyo tukufu ya Mtume (saw) ni safari ya Mtukufu huyo kutoka Makka, kitovu cha Uislamu kuelekea Baitul Muqaddas, kitovu cha dini za Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Mwandishi Sayyid Qutb wa Misri anasema: "Israa" yaani safari ya Mtume Muhammad (saw) kutoka Makkah hadi Baitul Muqaddas, iliunganisha dini zote kubwa za Tauhidi kuanzia dini ya Nabii Ibrahim na Ismail (as) hadi dini ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezu Mungu (saw), na kuyaweka pamoja maeneo matukufu ya dini ya Tauhidi. Kwa safari hiyo ya usiku, Nabii Muhammad alitangaza kuwa, risala na ujumbe wake ni mwendelezo wa ujumbe na njia ya Mitume waliomtangulia."
Imam Ja'far Swadiq (as) ambaye ni mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) anasema kuhusu safari ya Miiraji kwamba: Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu alipopelekwa Miiraji alipitia Baitul Muqaddas. Malaika Jibrilu alimpandisha juu ya Buraqi na kuandamana naye hadi Baitul Muqaddas. Jibrilu alimuonesha Mtume Muhammad (saw) mihrabu za Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu, na Mtume (saw) akaswali katika mihrabu hizo."
Kutokana na nafasi maalumu ya kidini ya mji huo mtakatifu na umuhimu wake katika dini ya Uislamu, daima Waislamu wamekuwa wakiupa heshima maalumu na nafasi ya tatu kwa utukufu baada ya miji ya Makka na Madina.
Mwaka wa 15 Hijria (636) jeshi la Waislamu lilielekea Baitul Muqaddas baada ya kukomboa Sham. Jeshi hilo liliuzingira mji huo kwa kipindi cha miezi minne na kukabiliana na mashaka makubwa hadi lilipofanikiwa kuukomboa bila vita wala mauaji. Watawala wa Baitul Muqaddas ambao walikuwa wamepoteza matumaini ya msaada wa Warumi na wakazi wake ambao walikuwa wamechoshwa na udhaifu na utawala mbaya wa viongozi wao, walipendekeza kwamba, mji wa Baitul Muqaddas ukabidhiwe kwa Khalifa na mtawala wa Waislamu. Jeshi la Waislamu pia lilikubali sharti la wakazi wa mji huo na kupeleka taarifa kwa Khalifa wakimtaka aelekee katika eneo hilo kwa ajili ya kukabidhiwa mji huo mtakatifu. Kwa ushauri wa Imam Ali bin Abi Twalib na vigogo wengine wa Madina, Khalifa na mtawala wa Waislamu wa zama hizo alielekea Baitul Muqaddas na kukutana na maaskofu na viongozi wa kidini kisha akaandika hati ya kuwadhaminia amani na usalama, na Baitul Muqaddas ikakabidhiwa kwake. Baada ya hapo Waislamu waliujenga upya mji huo mtakatifu ambao ulikuwa umeharibiwa na kufanywa magofu.
Miongoni mwa majengo muhimu ya kidini ya mji wa Baitul Muqaddas ni Msikiti wa al Aqsa ulioko upande wa mashariki wa mji huo ukielekea kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu ya al Kaaba, kibla cha Waislamu. Msikiti huo haukuwa kama ulivyo hivi sasa kabla ya kudhihiri dini ya Uislamu. Maeneo yote ya Haram ikiwemo Qubatu Sakhrah (قبةالصخرة) (The Dome of the Rock) yalihesabiwa kuwa sehemu ya Msikiti wa al Aqsa. Hata hivyo hii leo msikiti mkubwa uliopo kusini mwa uwanja wa Haram ndio unaopewa jina hilo. Ujenzi wa jengo jipya la Msikiti wa al Aqsa ulianzishwa mwaka 74 Hijria na mtawala Abdul Malik bin Marwan na kukamilika katika mwaka wa kwanza wa utawala Waliid bin Abdul Malik. Urefu wa msikiti huo ni mita 88 na upana wake una mita 55 na umejengwa katika ardhi yenye ukubwa wa mita 4400 za mraba. Mwandishi wa Kifaransa Gustave Le Bon ameandika katika kitabu cha The World of Islamic Civilization kwamba: "Msikiti wa al Aqsa ni miongoni mwa majengo muhimu zaidi na ya kustaajabisha yaliyojengwa na mwanadamu na umaridadi wake hautasawariki."
Qubbatu Sakhrah (قبةالصخرة ) (The Dome of the Rock) ni miongoni mwa athari muhimu za Kiislamu za mji wa Quds (Jerusalem). Miiraji ya safari ya kelekea katika ulimwengu wa malakuti ya Mtume Muhammad (saw) ilianzia katika mwamba ulioko katika eneo hili. Jengo hilo lilijengwa na kukamilishwa mara mbili mwaka 72 na 78 Hijria katika zama za utawala wa Abdul Malik bin Marwan. The Dome of the Rock au قبةالصخرة iko umbali wa mita 500 kutoka Masjidul Aqsa. Msomi mmoja wa Ulaya anasema: "Nimeona na kushuhudia majengo mengi huko India na Ulaya lakini hadi sasa zijawahi kuona jengo maridadi na zuri kuliko Qubbatu Sakhrah." Mbali na majengo hayo mawili, kuna majengo mengine mengi ya kiutamaduni na kidini kama misikiti, madrasa na turathi za Kiislamu katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) ambazo zinaakisi adhama, maendeleo na ustaarabu wa Waislamu katika karne zilizopita. Misikiti 36 ya kale, makaburi ya Masahaba wa Mtume Muhammad (saw) kama kaburi la Ubada ibn Al-Samit al Ansari aliyekuwa kadhi wa kwanza Mwislamu katika mji wa Baitul Muqaddas, Hospitali ya Fatimi, Qubbatul Miiraj, Darul Hadith, Darul Qur'ani na kadhalika ni miongoni mwa vielelezo muhimu vya Kiislamu vya mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem).
Baitul Muqaddas (Jerusalem) ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi mwishoni mwa karne ya 5 Hijria. Hata hivyo utawala na usimamizi mbovu wa baadhi ya watawala Waislamu, udhaifu, kuporomoka na migawanyiko na hitilafu zilizojitokeza baina ya Waislamu viliimarisha nafasi ya maadui zao. Mwaka 490 Hijria Watu wa Msalaba (Crusaders) walikusanya jeshi kubwa katika maeneo yote ya Ulaya na kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Baitul Muqaddas. Jeshi hilo la Msalaba lilitumia njia za kikatili kupita kiasi na hatimaye likauteka na kuukalia kwa mabavu mji huo. Jeshi al Msalaba liliua Waislamu laki moja katika eneo la Haram tukufu ya Msikiti wa al Aqsa peke yake. Katika kipindi chote cha miaka 91 ya kukaliwa kwa mabavu Baitul Muqaddas na Msikiti wa al Aqsa, msikiti huo ulikaribia kuwa gofu na kuharibika kabisa hadi Kamanda Salahuddin Ayyubi alipoukomboa mji wa Akka mwaka 583 Hijria na kuelekea Baitul Muqaddas. Salahuddin Ayyubi aliukomboa mji huo mtukufu kutoka kwenye makucha ya wapiganaji wa Jeshi la Msalaba tarehe 17 Rajab mwaka 583 Hijria. Baada ya kukomboa mji huo, Ayyubi alitoa hotuba ndani ya Msikiti wa al Aqsa na akauosha kwa uturi baada ya kuukarabati na kuusafisha. Salahuddin Ayyubi pia aliweka humo minbari maridadi na nzuri kutoka Sham.