Oct 09, 2018 11:20 UTC

Miongoni mwa maswali yanayoulizwa kuhusu siku ya Ashuraa ni kwamba, je, Imam Hussein alikuwa na habari juu ya masaibu yatakayompata huko Karbala na kwamba atauawa shahidi katika mapambano hayo?

Kama jibu ni ndiyo, je, kwa nini hakufanya jitihada za kuokoa nafsi yake kutokana na mauti na mauaji hayo? Je, Mwenyezi Mungu si amesema katika aya ya 195 ya Suratul Baqarah kwamba: Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo?

Hapa tupaswa kusema kuwa, Mtume (saw) na Maimamu katika kizazi chake kitoharifu wamepewa elimu ya baadhi ya matukio ya ghaibu yatakayotukia katika siku za usoni. Hili pia si jambo makhsusi kwa Mtume wetu Muhammad (saw) bali pia Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu walipewa elimu kama hiyo ya baadhi ya mambo ambayo yalikuwa ghaibu kwa umma lakini yakafichuliwa kwa watukufu hao. Ghaibu au elimu ya ghaibu ina maana ya kitu kilichofichikana au kisichojulikana. Yumkini jambo fulani likawa ghaibu kwa mtu fulani lakini likajulikana kwa mtu mwingine. Aya za Qur'ani tukufu pia zinaigawa elimu ya ghaibu katika sehemu mbili: Baadhi ya aya za kitabu hicho zinasisitiza kuwa, kuna elimu ya ghaibu ambayo ni makhsusi kwa Mwenyezi Mungu SW na hajui elimu na mambo hayo isipokuwa Yeye tu. Kwa mfano tu aya ya 59 ya Suratul An'aam inasema: Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu.

Aya nyingine za Qur'ani tukufu zinasema kuwa, kuna elimu ya ghaibu ambayo wamepewa mawalii na wateule wa Mwenyezi Mungu. Aya za 26 na 27 za Suratul Jinn zinasema: Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake. Isipokuwa Mtume wake aliyemridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake. Kwa msingi huo elimu ya ghaibu kwa ujumla ni makhsusi kwa Mwenyezi Mungu Mjuzi wa yote lakini anawapa Mawalii na Mitume wake baadhi ya elimu hiyo na kuwajuza mambo ya ghaibu yasiyojulikana kwa watu wengine kama tulivyoona katika aya hizo za Qur'ani tukufu. Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba amesema: Mwenyezi Mungu anayo elimu ambayo haijui isipokuwa Yeye kepe yake, na elimu nyingine ambayo huwapa Malaika na Mitume wake; ile aliyowapa Malaika wake na Mitume wake sisi (Ahlubaiti wa Mtume) tunaijua elimu hiyo."

Kuhusu tukio la Ashuraa kumepokewa hadithi nyingi katika vitabu vya wanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu za Shia na Suni zinazoonesha kuwa, wakati Muhammad bin Hanafiyya mwana wa Imam Ali bin Abi Twalib na ndugu yake Imam Hussein alipojua kwamba, Imam (as) alikuwa na nia ya kuondoka Madina alimwendea na kumbumkusha jinsi watu wa Kufa walivyovunja na kukiuka ahadi zao wakati wa Imam Ali bin Abi Twalib na kipindi cha Imam Hassan al Mujtabaa (as) na kumshauri asielekee Iraq. Imam Hussein alimjibu kwa kusema: Nimemuona babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwenye ndoto akiniambia: Hussein nenda Iraq. Mwenyezi Mungu anataka kukuona umeuawa."

Mitume waliotangulia, Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as) walikuwa na habari ya yatakayojiri Karbalaa tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Imam Hussein mwenyewe pia alikuwa na habari ya jinsi atakavyouawa na nani watakaomuua, jinsi na wapi atakapouliwa. Kwa mfano tu imepokewa kutoka kwa Hudhaifa akisema: Imam Hussein (as) alisema: Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, Banii Umayyah watajumuika kuniuua mimi, na Umar bin Saad ataongoza jeshi litakaloniua. (شیخ حرّ عاملی، اثبات الهداة، ج5، ص 207) Vilevile imepokewa kwamba, mke mwema wa Mtume Muhammad (swa) Ummu Salamah radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema kwamba, Malaika Jibrail alimpasha Mtume (saw) habari ya jinsi Hussein atakavyouawa shahidi na akamkabidhi Mtume udongo wa ardhi ya Karbala. Mtume (saw) alilia sana baada ya kupewa habari hiyo na alinipa mimi udongo huo kama amana na kuniambia: Wakati wowote utakapoona umekuwa na rangi ya damu jua kwamba mwanangu Hussein ameuawa shahidi. Hadithi hii imepokewa katika vitabu vya historia na hadithi vya wanazuoni wa Shia na Suni. 

المعجم الکبیر، ج 3، ص 114، ح 2813؛ کفایة الطالب، ص 426؛ تهذیب الکمال، ج 6، ص 480؛ مجمع الزوائد، ج 9، ص 189؛ تهذیب التهذیب، ج 2، ص 346؛ الصواعق المحرقة، ص 292؛ ذخائر العقبی، ص 146؛ الخصائص الکبری، ج 2، ص 125؛ طرح الترتیب، ج 1، ص 41، طبق احقاق الحق، ج 11، ص 347 والکامل فی التاریخ، ج 4، ص 93. 

Vilevile Ibn Abbas anasimulia kwamba, Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib alipofika eneo la Karbala wakati wa kuelekea katika vita vya Siffin alisimama na kulia sana hadi ndevu zake zikaloa kwa machozi. Baada ya hapo alitueleza jinsi watoto wake watakavyouawa shahidi kidhulma na watu waovu katika eneo hilo.

Kwa msingi huo Imam Hussein (as) alikuwa akijua yote yatakayotokea Karbala siku ya Ashuraa. Sasa swali ni kwamba, pamoja na kwamba alikuwa akijua masaibu na mashaka atakayokumbana nayo kwa nini aliridhia kuelekea kwenye makucha ya mauti?

Ni kweli kwamba, Imam alijua kwamba atauliwa lakini wakati huo huo ni kiongozi na imam wa umma. Hivyo anapaswa kuishi kwa namna ambayo atakuwa kigezo na ruwaza njema kwa Waislamu na umma mzima. Kama Imam Hussein na mawalii wa Mwenyezi Mungu wangeamua kuishi na kutatua matatizo yao kwa kutumia elimu ya ghaibu waliyopewa na Mola Muumba na kustafidi na kitu ambacho watu wengine hawakupewa, basi hawawezi tena kuwa vigezo bora na ruwaza njema za kuigwa na kufuatwa na Waislamu. Vilevile itakuwa vigumu kwao kuwalingania watu kuwa na subira, kujisabilia na kupigana jihadi katika njia ya Allah SW. Kwa msingi huo Mtume na Maimamu watoharifu katika kizazi chake daima walikuwa wakitumia nyezo za kawaida katika maisha yao ya kila siku na si elimu ya ghaibu na miujiza isipokuwa pale ilipokuwa lazima na dharura kutumia nyenzo na mambo hayo kwa ajili ya kulinda dini na kuwaongoza watu.   

Kuhusu swali kwamba, Qur'ani inatukataza kujitumbukiza wenyewe katika maangamizo, inatupasa kusema kuwa, kuna tofauti kubwa baina ya kufa shahidi na kujitupa wenyewe kwenye maangamizo na kumwaga damu zetu sisi wenyewe bila ya lengo na faida. Kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika jihadi na kupigania Uislamu, dini na matukufu ya kibinadamu si kujitumbukiza katika maangamizo na suala hilo bila shaka lina faida na maslahi makubwa kwa Uislamu na wanadamu kwa ujumla.

Pili ni kwamba, katika dunia hii kuna malengo matakatifu ambayo kuna ulazima wa kusabilia roho na kila lililoghali kwa ajili ya kuyalinda na kuyatetea. Kwa mfano wanahistoria wanasema kuwa, Imam Ali bin Abi Twalib alikubali kulala katika kitanda cha Mtume (saw) usiku wa Hijra ya mtukufu huyo kuelekea Madina wakati washirikina walipokuwa wamezunguka nyumba ya Mtume wakisubiri kumshambulia mtukufu huyo wakati wa usiku na kumuua. Mwenyezi Mungu alimpasha Mtume wake siri hiyo ya makafiri wa Makka kupitia kwa Malaika Jibrilu na Mtume akamtaka Imam Ali alale kitandani kwake, na yeye mwenyewe akaondoka usiku wa manane. Wakati washirikina wapovamia na kuinua panga zao kwa ajili ya kumuua Mtume waliona kuwa aliyelala hapo alikuwa Ali bin Abi Twalib. Hapa Imam Ali alikuwa tayari kusabilia roho na uhai wake kwa ajili ya kulinda uhai wa Mtume (saw) na dini ya Uislamu ambayo ni malengo aali na matukufu zaidi. Hivyo hivyo Imam Hussein (as) alisabilia roho, watoto, ndugu, masahaba na vipenzi vyake katika siku ya Ashuraa mwezi Muharram mwaka 61 Hijria kwa ajili ya malengo aali na matukufu na akaunywesha mti wa Uislamu kwa damu yake safi na iliyotakasika. Kwa hakika hatua ya Imam Hussein (as) ilikuwa dhihirisho kamili la aya ya 207 ya Suratul Baqarah inayosema: Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.  

Tags