Zaynab SA Nuru ya Ahlul Bayt wa Mtume + Sauti
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika makala hii maalumu tuliyokuandalieni kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi Zaynabul Kubra SA. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa makala hii.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: "Thamani na adhama ya Bibi Zaynab SA inatokana na msimamo na harakati yake adhimu ya kibinaadamu na Kiislamu na kutekeleza kwake majukumu yake katika njia ya Mwenyezi Mungu... Zaynab SA hakuwa mwanamke aliyejiyeweka mbali na elimu na maarifa. Alikuwa na elimu kubwa zaidi na maarifa safi zaidi. Katika ile saa ya mgogoro (huko Karbala) hata watu wenye nguvu sana walishindwa kujua cha kufanya, lakini yeye alijua nini cha kufanya na ndio maana alimuunga mkono vilivyo Imam wa zama zake..." Mwisho wa kunukuu.
Hivi sasa tumo katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi huyo mtukufu ambaye aliwasha moto wa hasira dhidi ya batili na hivyo kuuparaganya ulimwengu wa madhalimu. Huyo ni Bibi Zaynab SA ambaye ni nuru na mwanga wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Alikuwa ni binti wa Imam Ali AS na mama yake ni Bibi Fatimatuz Zahra SA binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Alikuwa ni umbu yaani ndugu wa baba mmoja mama mmoja wa Hasan na Husain mabwana wa vijana wa watu wa peponi. Bibi huyo mtukufu alisimama kidete kutekeleza majukumu yake katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi na ukakamavu mkubwa katika kipindi kizito na kigumu sana na kupelekea athari za mapambano yake zibakie milele. Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi Zaynabul Kubra SA kama njia ya kuonesha mapenzi yetu makubwa kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayti wake, tukimsalia na kuombea rehema na amani Bwana Mtume Muhammad na Aali zake na tunakukaribisheni kusikiliza machache kuhusiana na mjukuu huyo mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ajaalie dua za wafanya ziara kutoka pembe mbalimbali za dunia katika Haram ya Bibi huyo mtukufu huko Damascus, Syria zitakabaliwe; na Mwenyezi Mungu auzime moto wa chuki na bughdha za maadui katika ardhi hiyo ya Waislamu.
اللهم صل علی محمد و آل محمد
Wakati binti wa kwanza kabisa wa Imam Ali AS na Fatimatuz Zahra SA aliofungua jicho kwa mara ya kwanza hapa duniani, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa safarini. Wazazi hao wawili walisubiri hadi Bwana Mtume arejee ili atoe jina la mtoto huyo kama alivyotoa majina ya kaka zake wawili, Hasan na Husain AS baada ya kupokea wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Aliporejea safarini, Bwana Mtume alikwenda nyumbani kwa nuru ya jicho lake, Bibi Fatimatuz Zahra SA. Imam Ali AS alimchukua mtoto huyo na kumpeleka kwa babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al Mustafa SAW. Bwana Mtume alikibusu kitoto hicho kichanga na kukipa jina la Zaynab. Baada ya hapo akagusanisha uso wake mtoharifu juu ya uso wa kitoto hicho na macho yake yakabubujikwa na machozi. Wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kitu gani kinakuliza? Akasema: Mtoto huyu atakuwa pamoja na kaka yake Husain katika misiba itakayompata.
Bibi Zaynab SA alianza maisha yake katika mazingira ambayo yalikuwa kitovu cha ufanisi na ukamilifu wa mwanadamu. Kila leo alipata uhai mpya kutokana na upole, huruma na maarifa ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Bibi Zaynab aliishi na Babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka mitano, na alipendwa sana na babu yake. Bibi huyo mtukufu alipata bahati ya kupambika kwa nuru ya balagha ya baba yake Imam Ali AS na roho yake ilifika kwenye ufukwe wa utulivu kwa malezi yaliyojaa mapenzi ya mama yake Bibi Fatimatu Zahra SA. Hiyo ilitosha kumfanya Bibi Zaynab SA kushehenezwa elimu na maarifa ya Mwenyezi Mungu na kupambika kwa fadhila kubwa za maadili bora.
Zaynab maana yake ni "pambo la baba" na hilo linaonesha nafasi na utukufu wa binti hiyo kwa baba yake Imam Ali AS. Waandishi wa kumbukumbu na historia za wapokezi wa hadithi yaani Ilmur Rijal, wamemtaja Zaynab SA kuwa mmoja wa wapokezi wakubwa na waaminifu sana wa Hadithi katika ulimwengu wa Kiislamu. Bibi huyo mtukufu amepokea hadhithi kutoka kwa watu watukufu kama baba yake, Imam Ali AS, mama yake Bibi Fatimatuz Zahra SA na kwa masahaba wengine watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Bibi Zaynab SA alikuwa bibi mwenye elimu kubwa, mwenye balagha kubwa na fasaha wa maneno. Allama Sayyid Amin, mmoja wa wanachuoni wakubwa ameandika katika kitabu chake cha A'ayanush Shii'a "اعیان الشیعه" kwamba:
"Zaynab alikuwa Bibi mtukufu na mwenye sifa bora. Fadhila zake ni kubwa na zinajulikana waziwazi kiasi kwamba hakuna haja ya kuzitaja na kuziandikia kitabu. Alikuwa mwingi wa busara, mbora wa maadili, mwenye uwezo mkubwa wa kutoa hoja, mkakamavu moyoni na rohoni, mwenye ufasaha katika mazungumzo, umbuji wa kubainisha mambo kwa balagha kubwa utadhani ni baba yake Imam Ali AS ushahidi wa hayo ulionekana wazi wazi katika hotuba alizotoa huko Kufa na Sham. Lakini hakuna cha ajabu kutolewa hotuba kama hizo na mtu kama Bibi Zaynabul Kubra SA, kwani yeye ni katika matawi ya shajara toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW.
Shakhsia ya Bibi Zaynabul Kubra ilijengeka kwa namna ambayo fadhila na ukamilifu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na wazazi wake wawili watoharifu yaani Imam Ali AS na Bibi Fatimatuz Zahra AS zilionekana wazi wazi kwa bibi huyo mtukufu. Bibi Zaynabul Kubra alikuwa na sifa mbili kuu na muhimu ambazo alijifunza kutoka kwa babu yake Bwana Mtume na wazazi wake wawili nazo ni kuridhia na kujisalimisha kikamilifu mbele ya kudura na maamuzi ya Mwenyezi Mungu. Subira, shujaa, ufasaha na balagha katika mazungumzo ni miongoni mwa sifa zilizompambanua Bibi Zaynab na wanawake wengine na kufanya afanikiwe katika kutekeleza majukumu yake ya kibinaadamu na kimaanawi. Bibi Zaynab binti Ali bin Abi Talib alikuwa na ufahamu mpana wa mambo tangu utotoni mwake na alikuwa na roho iliyojaa elimu na maarifa na licha ya umri wake mdogo, lakini aliweza kuhifadhi vilivyo khutba ya kihistoria ya mama yake Bibi Fatimatuz Zahra SA aliyoitoa baada ya kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW na kuwanukulia watu wengine kama ilivyo. Katika zama hizo, wanawake walikuwa hawapewi nafasi kabisa ya kutafuta elimu na kustafidi nayo. Lakini binti huyo mdogo wa Imam Ali AS alifunzwa elimu na malezi ya Kiislamu na umashuhuri wa elimu yake ulienea maeneo ya mbali na karibu na mji wa Madina kiasi kwamba akinamama wengi walikwenda kwa Bibi Zaynab SA kusoma darsa za tafsiri ya Qur'ani. Bibi Zaynab alitumia fursa hiyo kueneza elimu ya Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW katika mji wa Madina na katika muda ambao baba yake Imam Ali AS alikuwa anaishi kwenye mji wa Kufa wa Iraq ya leo. Bibi Zaynab alitoa mchango mkubwa wa kuulinda Uislamu katika mapambano ya Karbala yaliyopelekea kuuawa shahidi Imam wa zama zake, Imam Husain AS na baada ya hapo alichukua jukumu la kumlinda Imam Sajjad AS ambapo hotuba za watukufu hao wawili huko Kufa na Sham zilitoa mchango mkubwa wa kuwaamsha watu na kufichua dhulma ya watawala madhalimu wa wakati huo.
Tunatumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu huyo mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kufuata vizuri sira ya bibi huyu mtukufu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.