Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu
Azimio la Milenia la Umoja wa Mataifa limeutangaza mshikamano kuwa ni miongoni mwa thamani za kimsingi katika mahusiano ya kimataifa katika karne ya 21.
Hii leo dunia inaendelea kutawaliwa na utandawazi huku ukosefu wa usawa ukizidi kuongezeka siku baada ya nyingine; kwa msingi huo inaonekana kuwa kuna udharura wa kuimarisha zaidi mshikamano wa kimataifa baina ya wanadamu. Kwa kutilia maanani hayo, mwaka 2005 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio lililoitambua tarehe 20 Disemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu ili kusisitiza umuhimu wa kuwepo mshikamano na kutokemeza umaskini na mashaka mengine katika jamii za wanadamu.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, Disemba 20 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu, ambayo Umoja wa Mataifa huitumia kusherehekea umoja miongoni mwa watu licha ya tofauti zao, husuani katika malengo ya pamoja kama maendeleo endelevu SDGs yanayowalenga watu na sayari ya dunia.
Ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu SDGs, ambayo imezingatia haki za binadamu na kuungwa mkono kimataifa, inalenga kuinua watu kutoka kwenye umasikini, njaa na magonjwa. Ajenda hii imejengwa katika msingi wa ushirikiano wa kimataifa na mshikamano baina ya watu.
Siku ya kimataifa ya mshikamano hutumiwa pia kuzikumbusha serikali kuhusu ahadi zao za kuheshimu makubaliano ya kimataifa na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa mshikamano.
Siku hii ni siku ya kuenzi mshikamano wa binadamu licha ya utaifa, mbari, rangi na kaumu zao tofauti. Kwa lengo hilo pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeanzisha Mfuko wa Kimataifa wa Mshikamano wenye lengo la kung'oa mizizi ya umaskini na kuzidisha ustawi wa kijamii katika nchi zinazostawi hususan zile zenye idadi kubwa ya watu maskini.
Itakumbukwa kuwa azimio la Milenia limepasisha suala la kutokomeza umaskini, kulinda sayari ya dunia na kudhamini utukufu na heshima ya wanadamu wote. Hati hiyo ya Umoja wa Mataifa imejikita zaidi katika masuala mawili muhimu yaani mwanadamu na sayari ya dunia na inasisitiza suala la kuokoa wanadamu wote ulimwenguni kutokana na umaskini, njaa na maradhi. Ni wazi kuwa mambo haya hayaweza kutimia isipokuwa kwa ushirikiano na mshikamano wa dunia nzima.

Azimio la Ustawi wa Milenia lililopasishwa mwaka 2000 limeutambua mshikamano kuwa ni thamani ya kimsingi katika mahusiano ya kimataifa. Kwa mujibu wa azimio hilo, changamoto za kimataifa zinapaswa kutatuliwa kwa njia ambayo gharama na majukumu ya suala hilo yazingatie misingi ya insafu na uadilifu wa kijamii. Watu wenye mashaka na wanaoshi katika tabu wanapaswa kusaidiwa na wale wenye hali nzuri ya kimaisha. Vilevile kuna udharura wa kuimarishwa zaidi mshikamano na ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kutimiza malengo ya milenia ya ustawi hususan katika zama hizi za utandawazi.
Miongoni mwa misingi ya awali ya Umoja wa Mataifa ni suala la kuonesha mshikamano na watu wanaosumbuliwa na umaskini na ukandamizaji. Chini ya kivuli cha mshikamano huo, wanadamu na serikali zina jukumu la kuhakikisha kwamba, uadilifu na usawa unatendeka katika jamii kwa ajili ya wanadamu wote. Mshikamano kama huu ndio unaoweza kuimarisha amani na usalama wa kimataifa.

Dunia ya leo inasumbuliwa na matatizo mengi ambayo hayawezi kutatuliwa na nchi moja. Vilevile nchi nyingi za dunia ya sasa zinasumbuliwa na umaskini na majanga ya kimaumbile kama mabadiliko ya hali ya hewa, uhaba wa chakula na maji safi, mafuriko, ukame, zilzala na kadhalika. Kwa sababu hiyo kuainishwa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu kunaweza kuwa fursa nzuri ya kuwakumbusha walimwengu mashaka na matatizo ya dunia ya sasa na kutafuta jinsi ya kukabiliana nayo. Katika siku hii pia kunafanyika semina, mikutano na vikao vingi vinavyosisitiza masuala kama vile kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini, kutayarishwa dawa na zana za tiba kwa ajili ya watu wenye haja, kuwasaidia waliopatwa na maafa ya kimaumbile, kuwezesha wanadamu wote kupata elimu, kupambana na umaskini, ufisadi na ugaidi na kadhalika.

Siku hii pia ina umuhimu mkubwa katika masuala ya upande wa kisheria na haki za binadamu kama haki ya kuwa na amani, haki ya kujiainishia serikali na utawala, haki ya kuwa na mazingira salama na kadhalika. Hapa pia linajadiliwa suala la haki ya wananchi wa Palestina ya kujiainishia mustakbali wao na kuwa na nchi huru.
Kwa kutilia maanani matatizo mengi yanayozuia utekelezaji wa haki za binadamu, mwaka 2005 Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilipasisha azimio lililopelekea kuteuliwa mtaalamu huru na wa kujitegemea katika masuala ya haki ya mshikamano ili aweze kufanya utafiti na kutayarisha azimio la haki za wanadamu kuhusiana na mshikamano wa kimataifa. Katika ripoti yake mtaalamu huyo alisema kuwa, ili kuweza kupatikana mshikamano wa kimataifa baina ya wanadamu kuna ulazima wa kuwepo ushirikiano wa wanachama wote wa jamii ya kimataifa. Alisema kuwa mshikamano ndilo sharti la kupatikana hadhi na heshima ya binadamu, msingi wa haki za kiumbe huyo na ustawi wake. Ripoti hiyo ilisisitiza kuwa mshikamano baina ya wanadamu unaweza kupatikana pale kila nchi itakaposhughulikia ipasavyo si matatizo ya raia wake pekee bali pia matatizo na mahitaji ya watu wa mataifa mengine.
Hii leo katika maeneo mbalimbali ya dunia tunashuhudia kwamba nchi nyingine zimetenga matukio na minasaba tofauti ya kila mwaka kwa ajili ya kuonesha mshikamano na watu wanaodhulumiwa au kukandamizwa kama vile siku ya mshikamano na wananchi wa Palestina au siku ya kuonesha mshikamano na watu wa Kashmir. Hatua kama hizi zinadhihirisha vyema zaidi umuhimu wa suala hili la mshikamano na ushirikiano baina ya jamii za wanadamu. Katika minasaba ya siku hizi hujadiliwa maudhui na masuala yanayoweza kuimarisha utamaduni wa amani, upendo, udugu na muawana baina ya wanadamu wote.
Mwishoni mwa kipindi hiki inatupasa kusisitiza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu ni nembo ya kutukumbusha na kutushajiisha zaidi kuhusiana na suala hilo muhimu na lenye thamani kubwa na wala suala hili la mshikamano baina ya wanadamu si makhsusi kwa siku moja tu ya mwaka. Katika siku hii ya kimataifa pia inatupasa kutathmini kazi na juhudi zote zilizofanyika katika nyanja za kimataifa kwa ajili ya kufikia malengo ya mshikamano na muawana kwa ajili ya kuboresha zaidi juhudi hizo na kurekebisha pale tulipokwenda mrama. Dunia ya leo ina idadi kubwa zaidi ya watu maskini kuliko matajiri, na vilevile idadi kubwa ya watu wenye mahitaji maalumu ambao wana hamu ya kutaka kuwa na maisha mazuri kama wengine. Muawama na mshikamano wetu na watu hao unaweza kuwa faraja kubwa kwa matabaka hayo. Vilevile tunapaswa kuelewa kwamba, kuwasaidia watu hao ni miongoni mwa sababu za maendeleo ya ustawi wa mataifa yote.