Kipindi maalumu cha ukumbusho wa kuuawa shahidi Bibi Fatiimah AS
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i58776-kipindi_maalumu_cha_ukumbusho_wa_kuuawa_shahidi_bibi_fatiimah_as
Mji mtakatifu wa Madina ulikuwa ungali unaomboleza kifo cha Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) ambapo msiba mwingine mkubwa uliukumba mji huo kutokana na kifo cha kushtua cha binti yake mwema Bibi Fatwimat az-Zahra (as).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2020 07:28 UTC
  • Kipindi maalumu cha ukumbusho wa kuuawa shahidi Bibi Fatiimah AS

Mji mtakatifu wa Madina ulikuwa ungali unaomboleza kifo cha Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) ambapo msiba mwingine mkubwa uliukumba mji huo kutokana na kifo cha kushtua cha binti yake mwema Bibi Fatwimat az-Zahra (as).

Mji huo ulikuwa ungali umetanda wingu jeusi la kuondokewa na mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Rehema kwa Walimwengu Mtume Muhammad (saw). Kila mmoja wa masahaba wa Mtume (saw) kwa mujibu wa kiwango cha imani na ikhlasi yake kwa Mwenyezi Mungu, alikuwa akihisi uchungu wa kuondokewa na Mtume lakini ni wazi kuwa mzigo mkubwa wa msiba huo ulihisika katika nyumba ya binti yake wa pekee, Bibi Fatwimah (as). Nam! huyu ni Fatwimah ambaye baba yake Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akimuita kwa majina ya 'Mama ya Baba yake' na 'Pande la Mwili wake'. Huyu Ni Zahra ambaye kila mara Mtume (saw) alipopatwa na hofu ya harufu ya Peponi, alikuwa akibusu na kumnusa binti yake huyo. Nam! Sasa binti huyu alikuwa amepatwa na msiba mkubwa ambao ulikuwa ukiendelea kuwa mzito zaidi siku baada ya nyingine. Msiba huo haukuwa mkubwa tu kutokana na kumpoteza baba yake mpenzi bali ulitokana pia na ukweli kwamba ujumbe wake ulikuwa ukielekea kusahaulika. Pamoja na hayo, Fatwimah alikuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya kuunusuru ujumbe huo wa Uislamu ambao ulikuwa unakaribia kusahaulika.

Jambo lililokuwa likimtatiza sana Fatwimah mbali na kumpoteza baba yake mpendwa, ni kudhihiri kwa pengo kubwa na upotovu katika jamii ya Kiislamu. Fatwimah alikuwa akiishi katika nyumba ambayo hata Mtume mwenyewe alipotaka kuingia humo, alikuwa akiomba idhini ya kufanya hivyo, lakini baada ya kuaga kwake dunia,  nyumba hiyo alivamiwa na wakazi wake kukosewa adabu na kupata vitisho vya kila aina. Bibi Fatwimah alipata majeraha makubwa ya kimwili katika hujuma na uvamizi huo kadiri kwamba alilazwa na hatimaye kuuawa shahidi kutokana na majeraha hayo. Katika hatua iliyojaa maana na kuchukizwa na hujuma aliyofanyiwa na maadui, alisihi na kumuusia mume wake Ali (as) amzike nyakati za usiku na katika sehemu isiyofahamika na watu, jambo ambalo lilithibitisha wazi kuwa hiyo ilikuwa aina fulani ya malalamiko dhidi ya upotovu wa jamii. Kabla ya kuaga dunia, Bibi Fatwimah (as) aliomba maji na kuchukua udhu, akavaa mavazi safi na ya kupendeza na kuketi akiwa ameelekea upande wa Kibla na kisha kuomba dua ifuatayo: 'Ewe Mwenyezi Mungu! Yajaalie mauti yangu yatakaponifika, yawe ni mfano wa kipenzi changu ambaye amewasili kutoka safarini, nami nilikuwa ninamsubiri kwa hamu kubwa afike! Ewe Mwenyezi Mungu! Nirehemu na kunifariji na uijalie roho yangu iwe pamoja na roho za watu waliotakaswa, moyo wangu uwe pamoja na nyoyo za watu wema, mwili wangu uwe kando ya miili mitakatifu na amali zangu ziwe miongoni mwa amali zilizokubaliwa.'

Binti huyu mwema wa Mtume Mtukufu (saw) aliaga dunia tarehe tatu Jamadu ath-Thani mwaka wa 11 Hijiria huku akiwa amewaachia Waislamu na walimwengu thamani kubwa zaidi na za kudumu milele. Kwa mnasaba huu mchungu wa maombolezo ya kumpoteza Bibi Fatwimat az-Zahra (as), binti mwema wa Mtukufu Mtume (saw), tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu na wapenzi wote wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw).

Umri wa binti huyo wa Mtume (saw) humu duniani ulikuwa mfupi sana, na wala haukupita miaka 18 tokea kuzaliwa kwake. Pamoja na hayo katika umri huo mfupi, maisha ya mtukufu huyo yalijaa fahari, misimamo thabiti na mafanikio makubwa ya thamani za Kiislamu kadiri kwamba kila Mwislamu alijivunia na kuvutiwa na mafanikio hayo. Katika kipindi hiki kifupi tutaashiria baadhi ya sifa za kuvutia za Bibi Fatwimah (as) ili kuwapa fursa wanawake wa leo wapate kuziiga sifa hizo katika maisha yao ya kila siku.

Moja ya sifa muhimu za Bibi Fatwimah (as) katika maisha yake ni daraja ya juu ya kimaanawi aliyokuwa nayo bibi huyo mtukufu. Alikuwa na takwa ya hali ya juu kiasi kwamba kila alilofanya na kusema lilizingatia kikamilifu sheria za Mwewnyezi Mungu na kwa lengo la kupata radhi zake. Jambo lililokuwa likimridhisha maishani ni kuona kuwa kila hatua aliyoichukua ilikuwa ni katika kuhudumia hakika na kwa madhumuni ya kumridhisha Mwenyezi Mungu Muumba. Daima alikuwa msaada mkubwa kwa baba yake katika mazingira magumu. Mtume alipokabiliwa na dhulma na maudhi tofauti ya mushrikina, Fatwimah daima alikuwa pembeni yake kutetea ujumbe wake (saw).

Siku moja Mtume Mtukufu (saw) alimuuliza binti yake Fatwimah (as) kwa kumwambia: 'Mwanangu Fatwimah! Una haja na ombi gani? Hivi sasa Malaika Jibril yuko pembeni yangu na ameleta ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili ujibiwe kila unalolitaka. Bibi Fatwimah alimjibu baba yake kwa kumwambia: Ladha ninayoipata katika kumuhudumia Mwenyezi Mungu inanizuia kumuomba jambo jingine lolote. Sina haja nyingine ghairi ya kutaka daima niwe ninautazama wema, uzuri  na ukarimu wake Mungu Mtukufu.'

Mtume (saw) anasema kuhusiana na binti yake huyu: 'Imani ya Mwenyezi Mungu imekita mizizi kwenye moyo wa Bibi Fatwimah ambapo ameachana na kila jambo kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu. Anaposimama kwenye mihrabu kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu, nuru yake huwameremetea watu wa mbinguni, na Mwenyezi Mungu kuwaambia Malaika: Hebu mtazameni mja wangu! Ni jinsi gani alivyosimamisha swala mbele yangu katika hali ambayo mwili wake wote unatetemeka huku akiwa amezama kwenye ibada! Enyi Malaika! Shuhudieni ya kwamba nimewaepusha wafuasi wa Fatwimah (as) na Moto wa Jahannam!'

Hadithi hii inabainisha wazi upeo wa hali ya juu wa kimaanawi wa wanawake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wanawake wa Kiislamu wanapasa kujifunza kutokana na Hadithi hii kwamba moyo wa ibada na uchaji Mungu unapatikana katika mienendo na vitendo vyao. Wanapasa kutumia baadhi ya wakati wao katika kusifu, kuhimidi, kuwaza na kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kutokana na imani na mtazamo wake wa kina, Bibi Fatwimah (as), baada ya Mtukufu Mtume (saw), alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwatahadharisha Waislamu kuhusiana na hatari ya kurejea katika utamaduni wa kijahili. Alikuwa akiamini na kusisitiza kwamba Qur'ani Tukufu na Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ndio njia ya pekee ya kumwokoa mwanadamu na kumletea saada ya humu duniani na ya kudumu milele huko Akhera.


Bibi Fatwimah aliunda familia na nyumba ambayo iliwavutia wengi katika historia ya Uislamu na daima ilijaa harufu ya umaanawi na usomaji Qur'ani Tukufu. Hakukuwepo na  alama wala nembo zozote za ujahilia, taasubi na sifa nyingine mbaya katika nyumba hiyo. Bibi huyo mtukufu bila shaka alikuwa uthibitisho kamali wa ukweli huu kwamba kufikia kilele cha umaanawi hakuhusiana na mwanamke au mwanaume tu. Hiki ni kipawa ambacho Mwenyezi Mungu amekiweka kwenye jinsia zote mbili ili waweze kunufaika nacho katika kuonyesha na kuuimarisha uwezo wao wa ndani. Bibi Fatwima pia alitumia muda wake mwingi kueneza elimu, maadili mema na utamaduni wa Kiislamu katika jamii.

Baada ya binti  huyo, mpendwa wa Mtume Mtukufu (saw) kutumia muda aliojaaliwa kuihudumia jamii na Uislamu, hatimaye muda wa kuondoka kwake humu duniani uliwadia. Licha ya Bibi huyo kukabiliwa na maumivu makali kutokana na majeraha aliyoyapata katika hujuma ya maadui nyumbani kwake, lakini bado aliendelea kutumia muda na fursa iliyosalia kumwabudu kwa ikhlasi Muumba wake Mtukufu. Bibi Asmaa  anasema kwamba katika nyakati hizo za mwisho za maisha yake duniani, alimwona Bibi Fatwimah akiwa amenyanyau mikono yake juu huku akimwomba Mwenyezi Mungu kwa baraka za baba yake Mtume Mtukufu, mumewe Ali (as) wanawe Hassan na Hussein (as) pamoja na mabinti zake, awahurumie na kuwasamehe watenda dhambi katika umma wa baba yake, kwa kuwa yeye Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Rehemu, Mwenye kurehemu.

Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw) kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka kuuawa shahidi binti ya Mtume Bibi Fatwimah (as), na tunamwomba Mwenyezi Mungu apate kutupa taufiki ya kuendelea kufuata njia ya binti huyo mtukufu, ambaye ni ua na pambo la Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw).