Dec 08, 2022 09:06 UTC
  • Maalumu Siku ya Kufa Shahidi Hadhrat Zahra al Batul (as)

Tarehe 13 Jumadil-Awwal, ni siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi binti wa Mtume wetu, Muhammad al Mustafa (saw), Bibi Fatimatu Zahra (as) na siku ya maombolezo ya Waislamu hususan wapenzi wa Ahlul Bait (as).

 Fatima Zahra (as) ndiye mwanamke bora zaidi ulimwengniu na kinara na kigezo bora cha kuigwa na wanawake. Kuna kauli mbili zilizopokewa kuhusu tarehe ya kufa shahidi kwa Hadhrat Zahra (as) baina ya wanachuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia. Kauli moja inasema mtukufu huyo aliaga dunia siku sabini na tano baada ya kufariki dunia baba yake, yaani Mtume Muhammad (saw), ambayo inasadifiana na tarehe 13 Jumadial-Awwal, na ya pili inasisitiza kuwa, aliaga dunia siku tisini na tano baada ya kifo cha kuhuzunisha cha baba yake, ambayo inasadifiana na tarehe 3 Jumadi al Thani.   

Hadhrat Fatima Zahra (as), ni binti wa Nabii Muhammad (saw) na Hadhrat Khadijah binti Khuwailid (sa), mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na mama wa Imam Hassan na Hussain (as). Bibi Fatima ana nafasi ya juu sana katika Uislamu na amepambwa kwa sifa nyingi. Baada ya mumewe, Ali bin Abi Twalib (as), maimamu wengine kumi na mmoja wa Ahlul Bait (as) wanatoka katika kizazi chake, na Sura na Aya kadhaa za Qur'ani kama vile Suratul Kauthar, Suratul Insan, Ayatu al Tat'hir, na Ayatul Mawaddah ziliteremshwa kuhusiana naye, mume wake na watoto wake.

Miongoni mwa Hadithi mashuhuri zinazohusiana na utukufu wa Bibi Zahra al Batul ni ile ya Mtume (saw) iliyopokewa katika Sahihi Muslim inayosema: 

"إِنَّ فَاطِمَةَ بَضْعَةٌ مِنِّی‏، مَنْ آذَاهَا فَقَدْ آذَانِی، وَ مَنْ غَاظَهَا فَقَدْ غَاظَنِی‏ وَ مَنْ سَرَّهَا فَقَدْ سَرَّنِی"

"Hakika Fatima ni sehemu yangu mimi, anayemuudhi huwa ameniumiza mimi, anayemkasirisha amenighadhibisha mimi, na anayemfurahisha amenifurahisha mimi." Vilevile Bukhari amepokea katika kitabu chake cha Sahihi Bukhari kwamba Mtume (saw) amesema: 

«فاطمة بضعة منی، فمن أغضبها فقد أغضبنی»

"Fatima ni pande la mwili wangu, anayemkasirisha huwa amenikasirisha mimi." Makusudio ya Mtume (saw) ni kwamba, mbali na kuarifisha na kueleza nafasi adhimu ya Fatima (as) mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, anatoa onyo na tahadhari ya kumdhuru, kumdhulumu na kumfanyia ubaya Hadhrat Fatima (as). Vilevile maana ya neno «بَضْعَةٌ مِنِّی‏» lililotumiwa na Mtume (saw) katika Hadithi hizi halina maana ya kipande cha mwili pekee; bali kama wanavyosema wanazuoni wengi waliofasiri Hadithi hizo ni kwamba Fatima ni sehemu ya roho, elimu, maarifa na maadili ya Mtume (saw) na ni kipande cha nuru na mwanga wa jua na mwangaza usio na mithili baina ya wanaadamu wa Mtume wetu Muhammad (saw).   

Inafaa kujua kwamba Mtume (saw) alikuwa na watoto wa kiume na wa kike wakati wa uhai wake. Kauli mashuhuri zaidi zinasema kuwa, mtukufu huyo alizaa watoto watatu wa kiume na wanne wa kike. Wa kiume walikuwa Qasim, Abdullah na Ibrahim, na wa kike ni Ruqayyah, Zainab, Ummu Kulthum na Fatima. Watoto wote wa Mtume (saw), isipokuwa Fatima (as), waliaga dunia wakati wa uhai wake, na Fatima al Zahra ndiye mtoto wake wa pekee aliyebakia hai hadi baada ya kuaga kwake dunia, na kizazi cha Mtume (saw) kimeendelea kupitia kwa Hazrat Zahra (a.s.). Kwa msingi huo, Mtume (saw) alifanya bidii kubwa kumpa malezi mema, na Zahra al Mardhiyya akafikia daraja kubwa hadi Mtume (saw) akampa jina la "Hurul Aini Mwanadamu" na "Sayyidatu al-Nisa" kwa maana ya kinara wa mbora wa wanawake wote,  na  "Ummu Abiha", yaani mama wa baba yake. 

Kwa kumpa majina na sifa hizi zote, Mtume Muhammad (saw) alitaka kuwalingania wanaadamu kwamba, Bibi huyu adhimu, ingawa ni mwanamke, lakini katika dunia nzima, hana kufu wala laiki isipokuwa Ali bin Abi Twalib (as), na kwamba kama si Ali hakuna mwanaume ambaye angeweza kuwa karibu ya Fatima (as). Hii ndiyo sababu Mtukufu Mtume (saw) akasema kwamba: "لَو لَمْ یُخْلَقْ عَلِیٌّ لَمْ یَکُنْ لِفاطِمَةَ کُفْوٌ" (Lau asingeumbwa Ali, Fatima asingekuwa na kufu).

Kumetajwa mengi kutoka kwa maimamu watoharifu kuhusu fadhila na matukufu ya Bibi Fatimatu Zahra (as). Imepokewa kwamba, Imamu Ja'far al Sadiq (AS) aliuliza: Je, unajua maana ya neno "Fatima"? Mpokezi wa Hadithi  akasema: Hapana, tafadhali nifahamishe tafsiri yake! Imam akasema: “Fatima” maana yake ni mtu ambaye shari na maovu hayafiki kwenye nafsi yake. Mwenyezi Mungu alimjaza bibi huyo kwa elimu na kumtakasa na machafu. Wallahi, Mwenyezi Mungu alimjaalia elimu kubwa kiasi kwamba, hakuhitaji elimu ya mwanadamu na wala hakuhitaji kujifunza kutoka kwa watu wengine, kwa sababu baba yake ndiye mwalimu wa kwanza wa Uislamu na Mtume wa Mwisho ambaye Mwenyezi Mungu alimtuma akiwa na dini kamilifu na  kitabu chake kitakatifu kwa wanaadamu." Alikuwa binti wa Mtume (saw), na watoto wake ni maimamu maasumu, kama Hassan na Hussein, ambao kila mmoja wao alikuwa hazina ya elimu na maarifa na wote walipata elimu kutoka kwa bibi huyo mtukufu.

Fatimatu Zahra (as) pia alikuwa na elimu na maarifa ya mambo mengi kupitia "elimu ya laduunni" ambayo Mwenyezi Mungu alimtunuku, na wakati wa uhai wake, Malaika walikuwa wakizungumza naye na kumjulisha masuala yatakayotukia baadaye. Kuhusiana na suala hilo Imam Sadiq (as) anasema: “Fatima, binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, alikuwa Muhaddatha (yaani mtu anayesemezwa na kuzungumzishwa na Malaika); Lakini hakuwa Nabii. Fatimah aliitwa Muhadathah kwa sababu Malaika walikuwa wakishuka kwake kutoka mbinguni na kuzungumza naye, kama ilivyokuwa kwa Bibi Maryam binti Imran, (mama yake Nabii Isa (as).

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, anasema kuhusu hali ya kiroho ya Bibi Fatima al Zahra (as) na jinsi alivyokuwa "Muhaddatha" kwamba: "Fatimatu Zahra (as) ni mtu ambaye alikuwa akizungumzishwa na maelfu ya Malaika wa karibu na Mwenyezi Mungu alipokuwa akisimama kwenye mihrabu ya ibada, wakimsalimu, kumpongeza na kumwambia maneno yaleyale yaliyokuwa yakisemwa na Malaika kwa Bibi Maryam mtakatifu.

Akitaja sifa na matukufu ya Zahraul Batul (as), Ayatullah Khamenei pia amesema: “Imepokewa katika Hadith kwamba, Hadhrat Maryam alikuwa kinara wa wanawake wa ulimwengu wa zama zake, lakini Fatima Zahra ni kinara na bibi wa wanawake wa ulimwengu katika vipindi vyote vya historia. Alifikia daraja za juu za kiroho kiasi kwamba Malaika walikuwa akizungumza naye katika kipindi cha ujana wake na kumfunza mambo mengi kwa kadiri kwamba alijulikana kuwa ni "Muhaddatha".

Bibi Fatima alijulishwa mengi hata kuhusu jinsi atakavyouliwa shahidi. Hadithi na nukuu za historia zinasema kuwa, katika saa za mwisho za uhai wake, alimjulisha mume wake, Ali bin Abi Talib (as) kuhusu kifo chake akisema: “Ewe Abal Hassan! Nimechukuliwa na usingizi kisha nikamuona kipenzi changu, Mtume wa Mwenyezi Mungu katika kasri la lulu nyeupe. Aliponiona alisema: Binti yangu! Njoo haraka kwa sababu nina hamu ya kukuona. Nimemjibu kwamba: Shauku yangu ya kukutana nawe, Yaa Rasullaha, ni kubwa zaidi. Wakati huo baba yangu alisema: "Utakuwa pamoja nami usiku wa leo"; na chochote anachoahidi yeye huwa ni mkweli na anatekeleza ahadi yake."

Bibi Fatimatu Zahra (a.s.) alisema wakati anamuaga mumewe, Amirul Muminin (as) kwamba: "Ewe Abul Hasan! Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliniahidi na kuniambia kwamba mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuungana naye, na hapana budi hili litatimia. Hivyo basi kuwa na subira mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mkubwa, na uridhiye hukumu yake."

Hapana shaka yoyote kwamba, hakuna mwanadamu anayejua wakati wa kifo chake isipokuwa akipewa ilhamu na Mwenyezi Mungu Mjuzi wa yote.

Mandhari ya kuuaga mwili wa Bibi Fatima, mbora wa wanawake wote duniani, ilikuwa ya kusikitisha sana. Imenukuliwa kwamba Imam Ali bin Abi Twalib na masahaba kadhaa waliokuwa karibu sana na familia ya Mtume waliuzika mwili wake usiku mkubwa kama alivyokuwa ameusia yeye mwenyewe, ili wale waliomdhulumu wasishiriki mazishi yake. Wakati anaweka mwili wake kaburini, Imam Ali (as) alisema maneno ya huzuni akimhutu Mtume (saw). Sehemu moja ya maneno hayo inasema:

السَّلَامُ عَلَیْکَ یَا رَسُولَ اللَّهِ عَنِّی وَ عَنِ ابْنَتِکَ النَّازِلَةِ فِی جِوَارِکَ وَ السَّرِیعَةِ اللَّحَاقِ بِکَ .... فَلَقَدِ اسْتُرْجِعَتِ الْوَدِیعَةُ وَ أُخِذَتِ الرَّهِینَةُ أَمَّا حُزْنِی فَسَرْمَدٌ وَ أَمَّا لَیْلِی فَمُسَهَّدٌ إِلَى أَنْ یَخْتَارَ اللَّهُ لِی دَارَکَ الَّتِی أَنْتَ بِهَا مُقِیمٌ وَ سَتُنَبِّئُکَ ابْنَتُکَ بِتَضَافُرِ أُمَّتِکَ عَلَى هَضْمِهَا فَأَحْفِهَا السُّؤَالَ وَ اسْتَخْبِرْهَا الْحَالَ

Sala na salamu za Allah ziwe juu yako Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kutoka kwangu na kwa binti yako anayekuja kwako na kuungana na wewe haraka... Amana uliyoniachia imereshwa, lakini huzuni yangu itabakia milele, na nyakati za usiku nitabakia macho hadi Mwenyezi Mungu atakaponichagulia nyumba yako unakoishi wewe kwa sasa. Binti yako atakupa habari kuhusu jinsi umma wako ulivyoungana kwa ajili ya kumdhulumu. Hivyo basi muulize yaliyojiri na yaliyotupata baada yako..... 

Tags