Feb 02, 2023 12:34 UTC
  • Nafasi ya Utawala wa Faqihi katika Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 44 wa ushidi wa Mapinduzi ya Kiislau ya nchini Iran.

Wasikilizaji wapenzi, kipindi chetu cha leo kitaangazia nafasi ya Utawala wa Faqihi na utawala wa mwanachuoni wa Kiislamu katika ushindi wa mapinduzi hayo matukufu. Tutaizungumzia fikra ya Utawala wa Faqihi kama nembo na siri ya ushindi wa Mapoinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1357 Hijria Shamsia yaani mwaka 1979 Milaadia. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Historia ya maisha ya mwanadamu inaonesha kwamba kutokana na migongano ya kimaslahi na tofauti za imani, wanadamu daima wamesimama dhidi ya kila mmoja wao katika pande mbili za haki na batili, na vita hivi vitaendelea hadi ushindi kamili wa haki dhidi ya batili, kama ilivyoelezwa ndani ya Qur'ani Tukufu. Vita hivi kati ya haki na batili vimeathiriwa na nguvu tofauti katika vipindi tofauti. Bila shaka, nguvu katika jamii zote zinatokana na shakhsia ya kiongozi wa jamii hiyo na nafasi yake. Kwa kufikia kwenye ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979, dhana ya uongozi na dhana ya madaraka kwa ujumla ilibadilika. Mabadiliko hayo yalitokana zaidi na aina ya uhusiano wa nguvu za hali ya juu kama vile kiongozi na wananchi wake, kwa sababu katika mchakato wa kufanikisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, uongozi ndani ya mfumo wa faqihi na mwanachuoni wa Kiislamu ulichukua nafasi kubwa zaidi ya ushindi wa Mapinduzi hayo matukufu ya Kiislamu. Kimsingi, moja ya mafanikio makubwa na muhimu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kuasisiwa mfumo wa kiutawala wa Kiislamu unaotokana na nadharia ya Faqihi Mtawala. Nadharia hii ya mwanachuoni wa Kiislamu kuwa mtawala imekuwa na nafasi ya kipekee si tu katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, bali pia katika kulivuusha taifa kwenye vipindi vigumu na vizito mno na kulifanya lishinde vikwazo na changamoto zote hizo.

 

Katika madh'hab ya Kishia, mbali na imani ya Tauhidi, Utume na Ufufuo, kuna itikadi nyingine mbili muhimu sana nazo ni Uadilifu na Uimamu. Msingi wa kisiasa wa itikadi hizo ni kwamba, baada ya kupita zama za Maimamu watoharifu (AS) na wakati wa ghaiba kubwa yaani wa kutokuwepo hadharani Imam Mahdi (AS) kwa muda mrefu, mtu anayestahiki zaidi, ambaye anapaswa kuwa kiongozi wa kusimamia masuala ya Waislamu, ni mwanachuoni mujtahid. Kwa mujibu wa nadharia hii, mafaqihi na wanazuini mujtahid ndio wanaochukua jukumu zito na la hatari la kuwaongoza Waislamu kwa niaba ya Imam maasumu. Faqihi na mwanachhuoni wa Kiislamu ndiye pekee anayeruhusiwa kubeba jukumu hilo zito la kusimamia utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu wakati wa kutokuwepo Imam maasumu. Kwa hivyo, Faqihi Mtawala ni istilahi mfumo wa serikali ya Kiislamu ya wakati wa kutokuwepo Imam Mahdi (AS) na nadharia ya Uongozi wa Faqihi maana yake ni kubebwa uongozi wa jamii ya Kiislamu na mtu ambaye amefikia nafasi ya ijtihadi katika fiqhi na ametimiza masharti ya kuongoza jamii ya Kiislamu. 

Kwa mujibu wa fikra za Kiislamu, kuwepo serikali katika jamii ni jambo la lazima na halijawekwa kwa ajili tu ya zama za kuwepo Mtume (SAW) na Maimamu maasum (AS). Upana na umilele kwa kanuni za Uislamu unahitaji kuwepo serikali katika zama za kutokuwepo Imam wa 12 wa Waislamu wa Kishia, yaani Imam Mahdi (AS) na unalifanja suala hilo kuwa jambo la lazima. Tukumbuke kuwa Mtukufu Mtume (SAW) aliwaita wanavyuoni kuwa ni makhalifa wake na warithi wa Mitume. Naye Imam Ali (AS) pia aliwahesabu wanavyuoni wa Kiislamu kuwa ni watawala wa watu. Imepokewa hadith kutoka kwa mtukufu huyo inayosema: “Kwa mujibu wa hukumu ya Mwenyezi Mungu na Uislamu kuhusu Waislamu, ni wajibu baada ya kifo au kuuawa kiongozi wao, awe kiongozi huyo ni mtu aliyepotoka au aliyeongoka, wasifanye chochote isipokuwa wachague mtu msafi, arifu na mcha Mungu kuwa kiongozi huyo. Wachague kiongozi ambaye ni mjuzi Hukumu za Mwenyezi Mungu Mungu na Mtume Wake ili aweze kusimamia vizuri mali za Waislamu, awezi kusimamia masuala ya Hija na kusalisha Sala za Ijumaa na wa kuweza kukusanya sadaka kwa ajili ya kuendeshea masuala ya Waislamu. Naye Imam Husain (AS) pia amesisitiza katika Hadith iliyonukuliwa kutoka kwake inayosema: "Vyanzo na mwelekeo wa mambo uko mikononi mwa wanavyuoni wa Mwenyezi Mungu. Kwani hao ndio wanaosimamia kiuaminifu halali za Mwenyezi Mungu na haramu Zake." Lakini pia kuna hadithi nyingine kutoka kwa Imam Mahdi (A.S.) ambayo inawabainisha waziwazi kwamba mafaqihi na wanafuoni wa Kiislamu ndio kuwa ni warithi wake katika zama za "ghaibatul kubra." Anasema: “Rejeeni kwa wapokezi wetu wa Hadithi katika mambo na matukio mbalimbali yanayotokea, kwani hao ni huja na wawakilishi wangu kwa ajili yenu na ni huja kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa hadithi hii adhimu, kila Muislamu anapaswa kurejea kwa watu wanaofahamu vizuri hadithi na mafundisho ya Uislamu katika mambo na matukio anakumbana nayo maishani. Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, "Utawala wa Faqihi" ndio msingi muhimu na mkuu wa nadharia ya kisiasa ya Uislamu wakati wa kutokuwepo hadharani Imam Mahdi (AS).

Imam Khomeini MA

 

Wakati wa kuundika Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) alichukua nafasi ya Faqihi Mtawala. Yeye ndiye nguzo ya Mapinduzi ya Kiislamu na ndiye aliyewaongoza wapambanaji hadi kufikia ushindi mapinduzi hayo matukufu. Ukuruba na huruma ya Imam Khomeini (MA) kwa watu, msimamo wake thabiti wa kupambana na uistikbari na mapambano yake yasiyochoka dhidi ya shulma na kuwatetea mno wanyonge, yote kwa pamoja yalimfanya Imam Khomeini kupendwa na jamii ya Kiislamu. 

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitokea wakati Marekani ilipokuwa inaongoza nchi za Magharibi huku Russia nayo ikiongoza nchi za Mashariki mwa dunia. Matukio yote duniani wakati huo lazima yalikuwa yanahusishwa na moja ya kambi hizo mbili, imma ya Magharibi au ya Mashariki. Lakini ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kilikuwa ni kitu kingine kabisa. Mapinduzi hayo hayakutegemea Magharibi wala Mashariki na hiyo ndiyo ilikuja kuwa kaulimbiu kuu ya wananchi wa Iran ya Si Mashariki, Si Magharibi bali ni Jamhuri ya Kiislamu. 

Wakati huo Imam Khomeini (MA) alitumia kigezo muhimu sana cha jihadi, kujitolea na kuwa tayari kufa shahidi katika njia ya Allah, yaani, Imam Ali (AS) na mwanawe mtukufu, Imam Husain (AS). Kwa upande mmoja, alilinganisha maisha yao ya kivitendo na hali ilivyokuwa wakati huo nchini Iran na katika upoande mwingine aliufananisha utawala wa wafalme wa Kipahlavi na utawala wa Yazid. Kwa kufanya hivyo, aliweza kumshama hisia na harakati za kimapambano za wananchi Waislamu na kuwafanya wasimame imara kupambana na utawala dhalimu wa Pahlavi.

Katika michakato yote inayojitokeza kwenye jamii za wanadamu, kutoka kwenye michakato iliyoandaliwa kitaasisi hadi katika michakato ya kijamii, kote huko kunahitajika uongozi, na kwamba nafasi ya uongozi ni ya kimsi na ya asili na haiwezi kufumbiwa macho bali haikanushiki katika masuala yote hayo. Moja ya mifano muhimu na madhubuti ya nafasi kubwa ya uongozi duniani ni usimamizi na uongozi wa maasi na mapinduzi ya wananchi yaliyotokea katika vipindi tofauti vya historia kwenye maeneo na sehemu mbalimbali duniani. Sambamba na hayo, moja ya sababu kuu za kuweza kufanikiwa malengo matukufu ya kila jamii, ni kuwa na utawala ulioshiakana vizuri na uongozi wa haki ambao unaisimamia na kuiongoza vizuri jamii ya Kiislamu. Kwa mujibu wa nadharia ya Kiislamu, Utawala wa Faqihi iwe ni upande wa kiongozi au upande wa wananchi, ni mfano wa tasbihi ambayo haikamiliki ila baada ya uzi na vilulu vyake viungane pamoja. Mpaka kongwa za mnyororo zote zishikamane vilivyo ndipo matilaba huweza kutimia. 

Uutawala wa Faqihi, siri ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Moja ya mafanikio muhimu na makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yameweza kuendelea kuwepo kwa mafanikio na kusonga mbele kwa zaidi ya miongo minne licha ya njama za kila namna za maadui ni nadharia ya "Walayatul Faqih," yaani Utawala wa Faqihi. Kwa kweli ni muhimu sana kuchunguza na kuchambua nafasi ya Imam Khomeini (MA) kama mtu ambaye aliweza kuitambua nadharia hii na kuipa nafasi yake inayostaki wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa fikra na mitazamo yake ya kipekee, Imam Khomeini (MA) alifanikiwa kwa taufiki ya Allah kuleta maadili ya kibinadamu na ya Kiislamu na kuwafanya watu wayatekeleze kivitando. Aliamshia na kuimarisha imani za wananchi wa Iran na kuwafanya wafanye kazi kwa bidii na kujitambua. Alihuisha maadili kama uhuru, kujikomboa, kupigania haki, kupiga vita dhuluma, udugu, kupenda na sifa nyingine nyingi aali za kimaadili. Pamoja na yote hayo lakini, huenda inaweza kusemwa kwamba mchango wake mkubwa zaidi kwa taifa la Iran na Waislamu wote duniani ni ubunifu wake wa kuunda serikali ya Kiislamu yenye msingi wa fiqhi ya Kiislamu. Tab'an mpango wa kuwa na serikali ya Kiislamu na masharti ya mtawala wa serkikali hiyo ulikuwepo kwa karne nyingi kati ya Waislamu wa Kisuni na Kishia. Lakini kipaji cha kipekee cha Imam Khomeini ni kwamba aliichambua kwa kina na kuitekeleza kivitendo fikra hiyo kwa uwazi kabisa na kwa kkutumia ushahidi wa kiakii na wa nukuu za Kiislamu. Kazi yake hiyo ilianza muda mrefu kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kitabu chake cha "Velayate Faqih" kwa hakika kinabainisha kwa uwazi suala hilo. Moja ya jumbe muhimu zaidi za msingi huo mtukukfu wa Kiislamu ni kuonesha kwamba dini hii ya Mwenyezi Mungu ina nafasi muhimu na kubwa katika masuala ya siasa tena nafasi kubwa sana.

Kama ilivyo maarufu kwa kila mtu, dini ya Kiislamu kwa sheria hizi za Bwana Mtume Muhammad SAW, ndiyo dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu na ndiyo dini ya kuunda serikali na kuendesha masuala ya jamii ya Kiislamu. Jamii ya Kiislamu siku zote inahitaji kuwa na mtawala na kiongozi wa kulilinda taifa la Kiislamu mbele ya shari za maadui wa Uislamu na Waislamu na kusimamisha uadilifu. Nadharia ya Faqihi Mtawala ni moja ya nadharia za kibunifu ambazo Imam Khomeini (RA) alizipendekeza na kuzifafanua kivitendo. Kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nadharia hii ikawa ndio msingi wa mfumo na wa serikali ya Kiislamu ya Iran, na baadaye ikawa ndiyo nguzo kuu ya kuhifadhika, kudumu na kuimarika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miongo iliyofuata.

Nafasi ya utawala wa mwanachuoni wa Kiislamu katika kuendeleza na kuimarisha Mapinduzi ya Kiislamu imedhihirika wazi kwenye kuongoza na kuchora sera jumla za nchi na pia katika kuzuia na kukabiliana na mizozo na njama za maadui. Kwa hakika, nadharia ya Uutawala wa Faqihi ni ngao ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni mdhamini wa kubakia mfumo huo mtukufu na kujikinga na hatari, mikengeuko na migogoro inayoweza kutokea. Kwa kweli haiwezekani kupatikana kinga hiyo bila ya kuwepo nguzo hii kuu na ya kimsingi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Uongozi uliojaa hekima na busara wa Imam Khomeini (MA) na Imam Khamenei (Mudda dhwilluhul 'Aali) unachora kwa vizuri mno nafasi ya Uongozi wa Faqihi katika muendelezo wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuimarika kwake. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu nafasi ya Uongozi wa Faqihi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwamba: “Uongozi wa Faqihi una nafasi ya uhandisi wa kuunda nakulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuhakikisha hauendi kombo na hautoki kwenye mstari sahihi. Kazi yake ni kulinda harakati kuu ya mfumo huo kuelekea kwenye malengo yake aali na matakatifu na hilo ndilo jukumu muhimu zaidi na la kimsingi zaidi za Uongozi wa Faqihi.

Tags