Jul 31, 2021 08:16 UTC
  • Ripoti: Mateka wa kike wa Palestina wanakabiliwa na hali mbaya katika jela za Israel

Kamati ya Masuala ya Mateka wa Palestina imetangaza kuwa mahabusu na mateka wa kike wa Palestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel wanaendelea kusumbuliwa na ukatili na hali ngumu kupita kiasi.

Taarifa iliyotolewa leo na kamati hiyo imesema kuwa, wahabusu wa kike wa Kipalestina katika korokoro za Israel wanaishi katika mazingira mabaya na magumu sana. Ripoti hiyo imeashiria hali ya mahabusu Muna Qaadan, mwanamke wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 50 aliyekamatwa na askari wa Israel miezi mitatu iliyopita akiwa nyumbani kwake na kufungwa jela. 

Ripoti ya Kamati ya Mateka wa Kipalestina katika korokoro za Israel inasema kuwa Muna Qaadan amekuwa akiteswa na kupewa manyanyaso ya aina mbalimbali kwa siku 22 mfululizo.

Taarifa ya kamati hiyo imesema kuwa, Muna ambaye hadi sasa ameshafungwa miaka 8 katika jela za Israel amesema kuwa, hali ya jela za utawala huo ni mbaya sana na kwamba wanawake wengine 40 wa Kipalestina wanaendelea kusulubiwa katika gereza la Damun na kwamba baadhi yao wamehukumiwa vifungo vya muda mrefu vikiwemo vya miaka 16 jela.

Wapalestina karibu elfu 4 na 800 wanashikiliwa katika mahabusu za kutisha za utawala haramu wa Isarel wakiwemo watoto 170.

Tags