Jun 26, 2016 15:13 UTC
  • Sudan Kusini yazidi kuzama katika dimbwi la vita vya ndani

Mapigano makali ya silaha baina ya jeshi la serikali na makundi ya waasi yameshadidi katika mji wa Wau ulioko katika jimbo la Bahr el Ghazal nchini Sudan Kusini.

Mapigano hayo ambayo yameongezeka tangu siku kadhaa zilizopita huko kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini yamesababisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimisha maelfu ya wengine kukimbia makazi yao.

Shirika la Msalaba Mwekundu limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya na mashaka makubwa yanayowapata watu wa eneo hilo na kuripoti kuwa, maelfu ya raia wamelazimika kuukimbia mji wa Wau.

Sudan Kusini inasumbuliwa na matatizo mengi ya kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kijamii na vilevile ukosefu wa miundombinu ya ustawi, hitilafu za mipaka baina ya wakazi wa ukanda wa kaskazini mwa nchi hiyo hususan yale yenye utajiri wa mafuta na makundi ya waasi.

Jana Jumamosi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alitoa taarifa akilaani mapigano yaliyozuka upya huko Sudan Kusini na amezitaka pande zinazopigana kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa shabaha ya kutatua hitilafu zao.

Tags