Aug 19, 2023 10:25 UTC
  • Rais wa Somalia: Tutaitokomeza al-Shabaab ndani ya miezi 5

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amesema lengo la operesheni za kijeshi zinazoendelea nchini humo ni kulitokomeza na kulisambaratisha kundi la kigaidi la al-Shabaab katika kipindi cha miezi mitano ijayo.

Rais Muhamud anatazamiwa ndani ya siku chache zijazo kuzindua awamu ya pili kampeni hiyo ya kulisambaratisha kundi hilo la kitakfiri katika mji Dhusamareb, ulioko katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Maelfu ya wanajeshi wa Somalia wamekusanyika mjini hapo wakisubiri kutumwa katika pembe mbalimbali za Somalia katika awamu ya pili ya operesheni kabambe za kuzima harakati za al-Shabaab.

Hata hivyo baadhi ya wadadisi wa mambo wametilia shaka uwezekano wa kusambaratishwa kwa kundi hilo ndani ya miezi mitano ijayo, kwa kutilia maanani kuwa lingali linafanya mashambulizi ya hapa na pale nchini humo.

Wanajeshi wa Somalia wameshadidisha operesheni zao dhidi ya ngome na maficho ya kundi hilo la kigaidi. Jana Ijumaa, Wizara ya Ulinzi ya Somalia ilitangaza kuwa magaidi 30 wenye silaha wa genge hilo wameuawa katika operesheni za jeshi la nchi hiyo zilizofanyika kwenye jimbo la Galguduud la Gholghdod katikati mwa nchi hiyo.

Rais Mohamud wa Somalia

Aidha mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, jeshi la Somalia lilitangaza kuua magaidi 100 wa al-Shabaab katika operesheni ya kijeshi iliyoiendesha kwenye eneo la Fima lililoko baina ya majimbo mawili ya Shabelle ya Kati na Galguduud katikati mwa nchi hiyo.

Somalia imekuwa ikipambana na ukosefu wa usalama tangu mwaka 1991 na imekuwa uwanja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi.

Genge la kigaidi lililofanya ukatili mkubwa ndani na nje ya Somalia ni la al-Shabaab ambalo limejitangaza kuwa ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida barani Afrika, na ambalo limekuwa likijaribu kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007 

Tags