Malumbano ya kisiasa Madagascar baada ya mripuko wa bomu
Katika siku ya sherehe za kitaifa, nchini Madagascar, kulijiri mripuko wa bomu mjini Antananarivo, mji mkuu wa nchi hiyo na kusababisha makumi ya watu kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Anthony Rakotoarison, mkuu wa idara ya usalama na intelejensia iliyo chini ya polisi ya Madagascar, amenukuliwa akisema kuwa, idadi ya watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye uwanja wa michezo wa Mahamasina mjini Antananarivo imefikia 50. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya duru zimearifu kujeruhiwa watu 89, huku watu tisa kati yao wakiwa katika hali mahututi. Rais Hery Rajaonarimampianina wa nchi hiyo sanjari na kuwatembelea wahanga wa hujuma hiyo, amesema kuwa tofauti za kimtazamo ndio sababu kuu ya tukio hilo. Naye Mahafaly Solonandrasana, Waziri Mkuu wa Madagascar ametangaza kuwa, muda punde baada ya kujiri hujuma hiyo, polisi ilichukua hatua za haraka za usalama mjini hapo. Shambulio la mjini Antananarivo limeshadidisha zaidi mivutano ya kisiasa nchini humo. Hii ni kusema kuwa, serikali na wapinzani wanatuhumiana kuhusika na tukio hilo la siku ya Jumapili. Serikali inawatuhumu wapinzani kwa kufanya njama za kuibua machafuko nchini humo, tuhuma ambazo zimepingwa vikali na mrengo wa upinzani nao. Guy Rivo Randroanarisoa, mwanasiasa wa upande wa upinzani amenukuliwa akisema kuwa, ni suala jepesi sana kwa serikali ya nchi hiyo kuwatuhumu wapinzani kuwa wanapanga njama za machafuko nchini. Kwa upande wake Omer Beriziky, waziri mkuu wa zamani wa Madagascar na ambaye pia ni mkosoaji wa serikali ya Rais Hery Rajaonarimampianina amesema kuwa, ni jambo lisilokubalika kutekelezwa jinai kama hiyo, kutokana tu na tofauti za kisiasa. Inafaa kuashiria hapa kwamba, mgogoro wa kisiasa nchini Madagascar ulianza kushadidi miezi kadhaa iliyopita. Tofauti za wanasiasa zimeongezeka kiasi cha kuufanya mrengo wa upinzani nchini humo kuitaka serikali iitishe uchaguzi wa mapema. Kwa muji wa ripoti, vyama vitano vya upinzani nchini humo sanjari na kuikosoa serikali ya Antananarivo, vimemtaja Rais Hery Rajaonarimampianina kuwa asiyefaa kuongoza nchi hiyo. Lalatiana Rakotondrazafy, kiongozi wa chama cha Uhuru, ametaka kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema nchini humo. Rakotondrazafy amesema kuwa, kusubiri hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2018, ni sawa na kulisukuma taifa hilo kwenye kitanzi. Kwa mujibu wa katiba ya Madagascar, uchaguzi wa mapema unaweza kuitishwa kwa sababu za ima rais kufariki dunia, kujiuzulu au kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na wabunge. Mwezi Disemba mwaka 2013, Rais Rajaonarimampianina alitoa ahadi ya kumaliza mgogoro mkubwa wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hiyo. Hata hivyo ikiwa ni mwaka wa tatu sasa, rais huyo bado hajafanikiwa kutatua matatizo ya kiuchumi ya taifa hilo na kinyume chake nchi hiyo imezidi kuandamwa na matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kisiasa. Ni kwa kuzingatia suala hilo ndipo wapinzani wakawa wanajaribu kumuondoa madarakani Rais Hery Rajaonarimampianina kwa kutumia kisingizio cha matatizo ya kiuchumi,.