Aug 30, 2023 04:40 UTC
  • Rais wa Tunisia apinga kuanzishwa uhusiano na Israel

Rais Kais Saied wa Tunisia amekanusha vikali madai kuwa taifa hilo lina azma ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Akizungumza na mabalozi wapya walioteuliwa kuiwakilisha Tunisia katika nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu, Rais Kais Saied amesema: Kwa wanaozungumzia (kuanzishwa) uhusiano wa kawaida (na Israel), nawaleza kuwa msamiati huo hauna maana yoyote katika kamusi yangu."

Amesema kadhia ya Palestina ina umuhimu mkubwa kwa taifa hilo, na kusisitiza kwamba kuna haja ya milki za Palestina kurejeshwa kwa wananchi wa Palestina.

Rais wa Tunisia ameeleza bayana kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika kamwe haitaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Watunisia katika maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina

Hii ni katika hali ambayo, katikati ya mwezi huu wa Agosti, Abdelkader Bengrina, Rais wa Harakati ya Ujenzi wa Taifa ya Algeria aliwataka Waalgeria waitazame kwa karibu Tunisia, baada ya wajumbe wa utawala wa Kizayuni kuitembelea Tunisia mara kadhaa, katika juhudi za kushinikiza kuanzishwa uhusiano wa pande mbili.

Aidha mapema mwezi huu, Bunge la Tunisia lilitangaza kuwa, Kamati ya Haki na Uhuru ya taasisi hiyo ya kutunga sheria imeanza kuandaa muswada wa sheria ya kujinaisha vitendo vya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Wananchi wa Tunisia wamekuwa wakilaani dhulma na mauaji ya wananchi madhulumu wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kila leo. Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ililaani hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na kuitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake mkabala wa Palestina. 

Tags