UN: Watu 183 wameuawa katika mapigano Amhara, Ethiopia
(last modified Wed, 30 Aug 2023 08:16:54 GMT )
Aug 30, 2023 08:16 UTC
  • UN: Watu 183 wameuawa katika mapigano Amhara, Ethiopia

Umoja wa Mataifa umesema kwa akali watu 183 wameuawa katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia.

Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa alisema hayo jana Jumanne mjini Geneva na kuongeza kuwa, "Tunatiwa wasiwasi na kuvurugika hali ya haki za binadamu katika baadhi ya maeneo ya Ethiopia. Watu 183 wameuawa tokea Julai katika mapigano baina ya jeshi na wanamgambo wa kundi la Fano." 

Afisa huyo wa UN ameeleza kuwa, kutangazwa kwa hali ya hatari katika eneo la Amhara mapema mwezi huu wa Agosti kumeshadidisha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Hurtado amesema watu zaidi ya 1,000 wametiwa mbaroni tangu serikali ya Ethiopi itangaze hali ya hatari ya miezi sita ili kukabiliana na ghasia zilizotokea Bahir Dar, Gondar, mji wa kihistoria wa Lalibela na miji mingine; ghasia ambazo zimesababisha vifo vya makumi ya raia.

Mapigano hayo makali yalizuka Julai kati ya Jeshi la Ethiopia (ENDF) na wanamgambo wa eneo la Fano wa Amhara juu ya uamuzi wa serikali wa kuunganisha vikosi vya kikanda katika polisi wa shirikisho au jeshi.

Wanamgambo katika eneo la Amhara

Hivi karibuni, serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa imekomboa miji mikubwa katika eneo la Amhara ikiwa ni pamoja na Bahir Dar, makao makuu ya eneo la Amhara kutoka kwa "magenge ya wanamgambo waasi", baada ya siku kadhaa za vita kati ya jeshi la serikali kuu na wanamgambo wa eneo hilo.

Mapigano hayo yaliyozuka tangu mwezi Julai katika eneo hilo la pili kwa ukubwa nchini Ethiopia kati ya wanamgambo wa Fano na Jeshi la Ulinzi la Ethiopia, yamegeuka kuwa mgogoro mkubwa wa kiusalama. Mgogoro huu unatajwa kuwa mkubwa zaidi wa usalama nchini Ethiopia tangu vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili katika eneo la Tigray linalopakana na Amhara mwezi Novemba mwaka jana.