Sep 23, 2023 14:08 UTC
  • Ethiopia: Tumeanza duru mpya ya mazungumzo na Misri na Sudan kuhusu Bwawa Kuu la Renaissance

Ethiopia imesema imeanza duru ya pili ya mazungumzo na Misri na Sudan kuhusu bwawa lenye utata lililojengwa na nchi hiyo kwenye mto Nile na kuwa chanzo cha mvutano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo matatu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imeeleza hayo leo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X na kubainisha kuwa, duru ya pili ya mazungumzo ya pande tatu kati ya Ethiopia, Misri, na Sudan kuhusu operesheni ya kila mwaka ya Bwawa Kuu la Ethiopia la Renaissance (GERD) imeanza leo, Septemba 23, 2023 mjini Addis Ababa.
 
Taarifa hiyo ya wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imeongezea kwa kusema: "Ethiopia imejitolea kufikia suluhisho la mazungumzo na la kirafiki kupitia mchakato unaoendelea wa pande tatu."
 
Mazungumzo ya muda mrefu kuhusu bwawa hilo tangu 2011 hadi sasa yameshindwa kuleta makubaliano kati ya Ethiopia na majirani zake wa chini ya Mto Nile.
 
Misri na Sudan zinahofia bwawa hilo kubwa lililoghrimu dola bilioni 4.2 litapunguza kwa kiasi kikubwa sehemu ya maji ya Mto Nile wanayopokea, na mara kadhaa wameiomba Addis Ababa isitishe kulijaza hadi makubaliano yafikiwe.
 
Kwa muda mrefu, Misri imekuwa ikiliona bwawa hilo kama tishio halisi, kwa sababu inategemea Mto Nile kwa asilimia 97 ya mahitaji yake ya maji.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kulia) na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi

Baada ya kuzozana kwa miaka kadhaa kuhusu suala hilo, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed walikubaliana mwezi Julai kukamilisha makubaliano ndani ya miezi minne, na kuanza tena mazungumzo mwezi uliopita Agosti.

 
Hayo yamejiri wakati mnamo mwezi huu, Ethiopia ilitangaza kukamilika kwa ujazo wa nne na wa mwisho wa Bwawa Kuu la Renaissance, na kukabiliwa na mjibizo wa haraka wa Cairo wa kulaani hatua hiyo ikisema imechukuliwa kinyume cha sheria.
 
Msimamo wa Sudan, ambayo kwa sasa inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, umeyumba katika miaka ya hivi karibuni.
 
Umoja wa Mataifa unasema, Misri inaweza "kukosa maji ifikapo 2025" na baadhi ya sehemu za Sudan, ambapo mzozo wa jimbo la Darfur kimsingi ulikuwa ni vita vya kuwania maji, zinazidi kukabiliwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.../
 

 

Tags