Jul 04, 2016 07:08 UTC
  • Muswada wa sheria ya usawa wa jinsia wazua mpasuko Somalia

Muswada wa sheria inayoshinikiza usawa wa jinsia nchini Somalia umeibua mjadala, malumbano na uhasama kati ya viongozi wa kidini na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo.

Muswada huo ambao ulipasishwa na Baraza la Mawaziri Alkhamisi iliyopita, unashinikiza juu ya wanawake kupewa haki sawa na wanaume katika nyuga za siasa na uchumi-jamii. Hata hivyo hisia tofauti zimeibuka baada ya kupasishwa muswada huo ambao unasubiri baraka za rais wa nchi; viongozi wa kidini wakiukashifu kwa upande mmoja, huku watetezi wa haki za usawa wa jinsia wakiuunga mkono kwa upande mwingine. Sheikh Bashir Ahmed Salad, Mwenyekiti wa Baraza la Kidini nchini Somalia SRC ameutulia shaka muswada huo na kusema kuwa unaunga mkono ndoa za jinsia moja na kuharamisha ukeketaji, utamaduni unaoenziwa na idadi kubwa ya jamii ya Wasomali, mbali na kutaka kupewa wanawake nafasi za juu serikalini, jambo ambalo viongozi hao wa Kiislamu wanadai eti linakinzana na mafunzo ya dini hiyo. Hata hivyo, Zahra Mohamed Ali Samatar, Waziri wa Masuala ya Wanawake na Haki za Binadamu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ameeleza kughadhabishwa kwake na msimamo huo wa viongozi wa kidini na kusisitiza kuwa, muswada huo umejikita zaidi juu ya kuwapa wanawake nafasi sawa za ajira na elimu na kwamba viongozi wa kidini wanaeneza propaganda ili usipate uungaji mkoni. Tayari kamati maalumu inayowaleta pamoja mawaziri na viongozi wa Kiislamu nchini humo imebuniwa ili kuvichambua vipengee vilivyo na utata kwenye muswada huo wa sheria ya usawa wa jinsia.

Tags