Rais wa DRC amfananisha Rais Kagame na Adolf Hitler
(last modified Sun, 10 Dec 2023 03:03:48 GMT )
Dec 10, 2023 03:03 UTC
  • Rais wa DRC amfananisha Rais Kagame na Adolf Hitler

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemshabihisha mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame na mtawala wa zamani wa Ujerumani ya Manazi, Adolf Hitler.

Akihutubia umati wa wafuasi wake katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa rais mashariki mwa nchi, Rais Tshisekedi amesema, “Namhutubu Rais Paul Kagame wa Rwanda na kumuambia hivi- madhali ameamua kuwa na mienendo kama ya Adolf Hitler kwa kuwa na malengo ya kibeberu (ndani ya DRC), naahidi kwamba atakuwa na hatima kama ya Adolf Hitler.”

Ameendelea kusema: Niliposhika hatamu za uongozi kama rais wa nchi hii, nilitoa pendekezo la kuishi kwa amani na majirani zetu. Lakini tatizo ni kuwa, baadhi ya majirani zetu wana macho makubwa zaidi ya matumbo yao, na hivyo ndivyo alivyo mwenzangu, Kagame.

Huko nyuma pia, Tshisekedi aliitaja Rwanda kama jirani muovu na kuituhumu nchi hiyo mwanachama mwenza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa inataka kufanya ukiritimba na kudhibiti rasilimali, hasa ya madini huko mashariki mwa DRC.

Waasi wa M23 wanaoyumbisha usalama mashariki mwa DRC

Mvutano kati ya majirani hao umeongezeka tangu kuzuka upya kwa harakati za wanamgambo wa M23 mwishoni mwa 2021 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku Kinshasa ikiituhumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi; madai ambayo Kigali imeyakanusha.

Mwishoni mwa Julai mwaka huu, Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilikanusha kile ilichotaja madai yasiyo na msingi ya nchi ya Kongo DR kwamba, wanajeshi wake walivuka mpaka na kuingia DRC, ambapo ripoti zilidai kwamba mwanajeshi wake mmoja aliuawa.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

 

Tags