Mahakama ya Ecowas yaamuru kuachiwa huru Rais wa Niger aliyepinduliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i106046-mahakama_ya_ecowas_yaamuru_kuachiwa_huru_rais_wa_niger_aliyepinduliwa
Mahakama ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) jana iliamuru kuachiliwa mara moja na bila masharti Rais aliyepinduliwa wa Niger Mohamed Bazoum.
(last modified 2023-12-16T03:22:11+00:00 )
Dec 16, 2023 03:22 UTC
  • Mahakama ya Ecowas yaamuru kuachiwa huru Rais wa Niger aliyepinduliwa

Mahakama ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) jana iliamuru kuachiliwa mara moja na bila masharti Rais aliyepinduliwa wa Niger Mohamed Bazoum.

Mahakama hiyo ya Ecowas jana iliamuru kurejeshwa kwa Bazoum, ambaye alipinduliwa mamlakani na jeshi Julai 26 mwaka huu ikisema kuwa bado ni Rais halali wa Niger. Mohamed Bazoum na familia yake wamekuwa kizuizini katika ikulu ya Rais wa Niger licha ya matakwa mbalimbali ya jumuiya ya Ecowas na nchi nyingine  kwa ajili ya kumuachia huru rais huyo aliyepinduliwa wa Niger. 

Itakumbukwa kuwa Bazoum mwezi Septemba mwaka huu aliwasilisha kesi katika mahakama ya Ecowas akihoji kuhusu kupinduliwa na jeshi, kutiwa nguvuni na kuwekwa kizuizni na viongozi wa kijeshi; ambapo alitaka kuachiwa huru na  kurejeshwa mamlakani kama Rais wa Niger.  

Aidha tarehe8 mwezi huu wa Disemba mahakama hiyo ya jumuiya ya Ecowas ilitupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na utawala wa kijeshi wa Niger uliotaka kuondolewa nchi hiyo vikwazo vilivyowewa na viongozi na serikali za magharibi mwa Afrika.