Bunge la Ethiopia larefusha 'hali ya hatari' eneo la Amhara
Bunge la Ethiopia jana Ijumaa lilirefusha muda wa hali ya hatari iliyotangazwa Agosti mwaka uliopita 2023 katika eneo linaloshuhudia mapigano la Amhara.
Rasimu ya azimio la kurefusha muda huo kwa miezi minne zaidi iliwasilishwa Bungeni na Gedion Timothios, Waziri wa Sheria wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Waziri huyo alisisitiza kuwa kuna udharura wa kuongeza muda huo wa hali ya hatari kwa ajili ya kudhibiti amani na usalama katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.
Eneo la Amhara nchini Ethiopia limeripotiwa kuendelea kushuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho na wanamgambo wa eneo hilo.
Ghasia hizo huko Amhara, ambalo ndilo eneo la karibuni zaidi lililozuka machafuko nchini Ethiopia, zilisababisha kutangazwa hali ya hatari mwezi Agosti mwaka jana.
Mwezi huo huo, Umoja wa Afrika uliitaka serikali ya Ethiopia kufanya mazungumzo na wanamgambo katika eneo la Amhara ili kupata suluhisho la amani.
Mapigano hayo makali yalizuka tangu Julai 2023 kati ya Jeshi la Ethiopia (ENDF) na wanamgambo wa Harakati ya Kitaifa ya Amhara FANO juu ya uamuzi wa serikali wa kuunganisha vikosi vya kikanda katika polisi ya shirikisho au jeshi.