Wanajeshi 115 wauawa katika mapigano Juba, Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10894-wanajeshi_115_wauawa_katika_mapigano_juba_sudan_kusini
Wanajeshi wasiopungua 115 wameuawa Sudan Kusini katika mapignao baina ya mirengo hasimu serikalini katika mji mjuu Juba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2016 10:26 UTC
  • Wanajeshi 115 wauawa katika mapigano Juba, Sudan Kusini

Wanajeshi wasiopungua 115 wameuawa Sudan Kusini katika mapignao baina ya mirengo hasimu serikalini katika mji mjuu Juba.

Ufyatuaji risasi uliibuka Ijumaa jioni karibu na ikulu wakati Rais Salvaa Kiir alipokuwa akifanya mazungumzo na hasimu wake wa zamani, makamu wa rais Riek Machar.

Wawili hao wanasema hawajui chanzo cha mapigano  baina ya wafuasi wa mirengo yao huku wakitoa wito wa utulivu.

William Gatjiath Deng, msemaji wa mrengo wa Machar jeshini, amesema mapigano yalijiri karibu na ikulu ya rais na kituo cha jeshi. Amesema wanajeshi 35 wa mrengo wa Machar wameuawa huku wengine 80 wa mrengo wa Rais Kiir nao pia wakipoteza maisha katika mapigano hayo. Deng amesema idadi ya waliofariki katika upande wa Machar huenda ikaongezeka kutokana na kuwa baadhi wamejeruhiwa vibaha. Upande wa Rais Kiir haujatoa taarifa yoyote kuhusu hali ya mambo mjini Juba.

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ukionyesha wasiwasi wake kuhusiana na mapigano hayo mapya huko Sudan Kusini.

Matukio hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, leo taifa hilo changa zaidi barani Afrika linaadhimisha miaka mitano ya uhuru wake. Hata hivyo sherehe rasmi zimefutwa kutokana na ukosefu wa fedha.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.