Mar 29, 2024 06:35 UTC
  • Watu 45 wafariki dunia katika ajali ya basi la wafanyaziara wa Pasaka nchini Afrika Kusini

Watu wasiopungua 45 wamefariki dunia nchini Afrika Kusini wakati basi lililokuwa limebeba wafanyaziara wa Pasaka lilipotumbukia kwenye daraja jana Alhamisi.

Idara ya Uchukuzi ya Afrika Kusini imesema, msichana wa miaka minane ndiye pekee aliyenusurika kwenye ajali hiyo iliyotokea katika jimbo la kaskazini-mashariki la Limpopo. Mtoto huyo amepata majeraha makubwa na amelazwa hospitalini.
 
Imeelezwa kuwa, dereva alipoteza udhibiti wa basi kwenye njia ya mlima karibu na eneo la Mamatlakala na kupelekea kuanguka umbali wa mita 50 na kuwaka moto baada ya kugonga ardhi.
 
Basi hilo lilikuwa likichukua wafanyaziara wa Pasaka kutoka Botswana kuelekea mji wa Moria, huko Limpopo.
 
Serikali ya Afrika Kusini mara nyingi hutoa jumbe za umma kuhusu usalama barabarani wakati wa likizo ya Pasaka, ambacho ni kipindi cha hekaheka nyingi na hatari hasa kwa kusafiri nchini humo. Zaidi ya watu 200 walikufa mwaka jana katika ajali wakati wa wikiendi ya Pasaka.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametuma salamu za rambirambi kwa Botswana na kuahidi msaada kwa nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Serikali ya mkoa imesema miili mingi iliungua moto kiasi cha kutotambulika na kubaki ndani ya basi hilo.

Waziri wa Uchukuzi wa Afrika Kusini Sindisiwe Chikunga amesema uchunguzi kuhusu ajali hiyo unaendelea na akatoa rambirambi zake kwa familia za waliofariki.

Kwa mujibu wa mashirika ya habari, Kanisa la Kikristo la Kizayuni lina makao yake makuu mjini Moria na ziara zake za Pasaka huvutia mamia ya maelfu ya watu kutoka kote Afrika Kusini na nchi jirani pia.

Huu ni mwaka wa kwanza wa safari ya Pasaka kuelekea Moria kufanyika tangu lilipozuka janga la Covid-19.../

Tags