Apr 16, 2024 02:14 UTC
  • Mwaka mmoja wa vita baina ya majenerali wa kijeshi Sudan, maelfu wauawa, mamilioni wakimbia

Vita vikali vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vimeshaua maelfu ya watu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya wengine. Vita hivyo vimeingia mwaka wake wa pili huku kukiwa hakuna dalili za kukomeshwa vita hivyo licha ya kuweko onyo la mara kwa mara la njaa kali inayotishia kuwaua wale ambao hawakuuawa kwa risasi za vita hivyo.

Tangu vilipozuka vita baina ya mejenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya wanajeshi, yaani Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) Aprili 15, 2023, wahanga wakubwa wa vita hivyo vya uchu wa madaraka ni raia wa kawaida.

Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema: "Hadi hivi sasa watu 14,790 wameripotiwa kuuawa huku idadi ya watu waliokimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan ikifikia milioni 8.2."

Majenerali wa kijeshi walioisababishia maafa makubwa Sudan

 

Kwa upande wake, Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli kwa Sudan amesema: "Vyama vinavyopigana Sudan vina wajibu wa kisheria wa kuwalinda raia, lakini vimeonyesha kutowajali raia wa nchi hiyo." 

Nalo Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limeonya kuhusu hali mbaya ya usalama wa chakula nchini Sudan na kuzitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano mara moja na kuruhusu kufika misaada ya kibinadamu kwa watu wenye shida na matatizo mengi yaliyosababishwa na vita hivyo.

Kwa upande wake, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilisema siku ya Ijumaa kuwa mgogoro wa njaa wa Sudan utazidi kuwa mbaya kama misaada ya chakula haitapelekwa haraka kupitia njia zote zinazowezekana za kibinadamu.