Apr 17, 2024 06:46 UTC
  • IOM: Wahamiaji 584 waliokolewa katika pwani ya Libya wiki iliyopita

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema katika ripoti yake ya jana Jumanne kwamba, wahamiaji 584 waliokolewa nje ya pwani ya Libya wiki iliyopita.

Sehemu moja ya taarifa ya shirika hilo la kimataifa imesema kuwa, kuanzia tarehe 7 hadi 13 mwezi huu wa Aprili, wahamiaji 584 waliokolewa na kurudishwa nchini Libya.

Taarifa hiyo aidha imetoa ufafanuzi zaidi kwa kusema kuwa, wahamiaji waliookolewa ni pamoja na wanawake 54 na watoto 25. Imeongeza kuwa, maiti sita wa wahamiaji hao waliokuwa wanasafiri kinyume cha sheria nao wamepatikana kwenye kipindi hicho cha wiki iliyopita ya baina ya tarehe 7 hadi 13 Aprili.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, jumla ya wahamiaji haramu 4,942 wameokolewa, huku 143 wakifariki dunia na wengine 271 kutoweka kwenye pwani ya Libya.

Kwa sababu ya ukosefu wa usalama na machafuko nchini humo Tangu ulipoangushwa utawala wa zamani wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, wahamiaji wa mataifa tofauti, wengi wao wakiwa raia wa nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara wanatumia fursa ya kukosekana usalama, machafuko na kutokuweko serikali yenye nguvu nchini Libya, kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea kwenye fukwe za Ulaya kwa ndoto za kupata maisha bora. Lakini mara nyingine wanaishia kupoteza maisha baharini.