Apr 17, 2024 06:47 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasaidia kuwaokoa raia 5 waliotekwa nyara mashariki mwa DRC

Maafisa wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamesaidia kuwaokoa raia watano waliokuwa wametekwa nyara.

Msemaji Mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Stephane Dujarric ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, kikosi cha umoja huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kinachojulikana kwa jina la MONUSCO kiliingilia kati kusaidia kukombolewa raia watano akiwemo mwanamke mmoja na watoto wawili wachanga waliokuwa wametekwa nyara na kundi la watu wenye silaha karibu na eneo la Djugu katika jimbo la Ituri la mashariki mwa nchi hiyo. 

Aidha amesema: "Baada ya kukombolewa mateka hao, MONUSCO iliwapa makazi ya muda na msaada wa matibabu kabla ya kusafirishwa na maafisa wa timu hiyo na kurejeshwa makwao.

Hali ya usalama katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini inaendelea kuwa mbaya pia huku matukio ya kufyatuliana risasi yakiripotiwa tena kati ya wanajeshi wa serikali ya Kongo na waasi wa M23. 

Dujarric pia amesema, "Volker Turk, kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu ambaye hivi sasa yuko DRC kwa ziara rasmi kwa mwaliko wa serikali ya Kinshasa."

Turk ametembelea maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na kukagua kambi za wakimbizi wa ndani ambako alikutana na wapigania haki za binadamu na mashirika ya kiraia.

Msemaji huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema, huko mjini Kinshasa, Turk anatarajiwa kukutana na Rais Felix Tshisekedi, maafisa wakuu wa serikali na maafisa wenzake wa Umoja wa Mataifa.