Jun 23, 2024 09:19 UTC
  • Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinaendelea nchini Rwanda

Kampeni zilizoanza jana Jumamosi nchini Rwanda zinaendelea huku wagombea watatu waliopasishwa baada ya mchujo wa walijiandikisha kugombea wakizindua kampeni zao katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Wagombea watatu wanachuana kwenye kinyang’anyiro cha urais akiwemo rais wa hivi sasa Paul Kagame wa chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF). Wagombea wengine ni Frank Habineza wa chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda na Philippe Mpayimana, mgombea binafsi.

Wagombea tisa wa urais na karibu 700 wa ubunge waliwasilisha maombi yao ya kugombea lakini wamechujwa na kubakishwa wabombea watatu wa urais na 500 wa ubunge.

Kagame, mwenye umri wa miaka 66 na ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, alizindua kampeni zake wilayani Musanze, Mkoa wa Kaskazini, ambapo amezishutumu nchi za Magharibi kwa undumilakuwili na siasa zao za nyuso mbili kuhusu demokrasia baada ya madola hayo kumkosoa kwa kukaa muda mrefu madarakani. 

Rais Paul Kagame wa Rwanda katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi jana Jumamosi

 

Hivi sasa Kagame anawania kuchaguliwa tena baada ya marekebisho ya katiba ya 2015 ambayo yalimruhusu kugombea mihula mitatu zaidi. Mabadiliko ya katiba yalimruhusu Kagame kugombea muhula wa tatu wa miaka saba mwaka 2017. Lakini marekebisho mapya ya Katiba yanayoanza kutekelezwa mwaka huu wa 2024, yamepunguza muhula wa urais na kuufanya kuwa miaka mitano badala ya miaka saba nchini Rwanda.

Kwa upande wake, mgombea Habineza ameanza kampeni zake katika Wilaya ya Gasabo huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda, ambako alihutubia wafuasi wake wakati Mpayimana amezindua kampeni yake katika Wilaya ya Kirehe mashariki mwa Rwanda.

Wakati huo huo, kampeni zilizinduliwa katika maeneo tofauti ya nchi kwa zaidi ya wagombea 500 wa ubunge wanaogombea viti 80 bungeni. Uchaguzi wa rais na bunge wa Rwanda utafanyika Julai 15.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi takriban Wanyarwanda milioni 9.5 wametimiza masharti ya kupiga kura.