Jun 28, 2024 03:20 UTC
  • UN: Tumeshtushwa na mauaji dhidi ya waandamanaji Kenya

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa kwake na maandamano ya ghasia ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 nchini Kenya, yaliyopelekea makumi ya watu kuuawa.

Volker Turk ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi na kuwawajibisha waliohusika na mauaji hayo ya waandamanaji hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, Nairobi. 

Muswada huo umeibua maandamano makubwa ya Wakenya, ambapo polisi Jumanne iliyopita walikabiliana na waandamanaji huku watu wasiopungua 23 wakiuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema: Nimesikitishwa na mauaji na visa vya kujeruhiwa watu katika maandamano hayo. Natoa mwito wa kujizuia ili kuweka mazingira ya kutekelezwa haki ya kuandamana na kwa kujieleza kwa amani. 

Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa

Aidha afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kufanyika mazungumzo ili kusikiliza sauti na lalama za Wakenya hasa vijana.

Rais wa Kenya anakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi uliogubika uongozi wake wa miaka miwili; ambapo vijana nchini humo wa kizazi cha sasa (Gen Z) wanaongoza maandamano makubwa ya kupinga ongezeko la ushuru huku wakisisitiza kutekelezwa mageuzi makubwa ya kisiasa. 

Maandamano hayo makubwa ya siku kadhaa yaliyofuatiwa na mauaji ya waandamanaji mjini Nairobi Jumanne, yalimlazimisha Rais William Ruto wa Kenya kutotia saini muswada huo tata wa fedha 2024 kuwa sheria.

 

 

Tags