Jun 29, 2024 06:27 UTC
  • Rached Ghannouchi
    Rached Ghannouchi

Harakati ya Ennahda ya Tunisia jana Ijumaa ililaani kifungo cha kiongozi wake, Rached Ghannouchi, kutozwa faini, na kuwekwa chini ya udhibiti wa kiutawala kwa miaka 3.

Harakati hiyo imekariri wito wa kuachiwa huru Ghannouchi na wafungwa wote wa kisiasa nchini Tunisia.

Jumatatu iliyopita, Mahakama ya Rufaa nchini Tunisia ilitoa uamuzi dhidi ya Ghannouchi kwenda jela mwaka mmoja, faini ya dinari 1,000 ($333), na kumuweka chini ya udhibiti wa utawala (akiripoti polisi kila siku) kwa kipindi cha miaka 3.

Ennahdha imesema katika taarifa yake kwamba inalaani kuendelea kukamatwa kiongozi wake, adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela na miaka mitatu ya udhibiti wa kiutawala iliyotolewa dhidi yake, "katika kesi ovu ya mashtaka yasiyo na msingi."

Harakati hiyo imesema kwamba kinachomtokea Ghannouchi ni dhulma ambayo haikuzingatia hadhi yake, hali yake ya kiafya, na umri wake mkubwa. Imedokeza kuwa Ghannouchi amefikisha umri wa miaka 83 na anakaa gerezani mwaka wa pili katika siku yake ya kuzaliwa.

Ennahda imekariri matakwa yake ya kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa na kutishwa mashambulizi yanayowalenga wapinzani, wafungwa wa dhamiri, wanaharakati na wanablogu ambao wameonyesha msimamo wa kushikamana kwao na mafanikio ya ukombozi.

Ghannouchi anakanusha tuhuma za kutukuza ugaidi, na anasema kwamba kesi hiyo imeanzishwa kutokana na upinzani wake dhidi ya Rais Kais Saied wa Tunisia. Pia anakataa kufika mbele ya mahakama.