Pendekezo jipya la mfuko wa uwezeshaji laleta matumaini kwa wanawake wajane Afrika
(last modified 2024-07-08T03:40:08+00:00 )
Jul 08, 2024 03:40 UTC
  • Pendekezo jipya la mfuko wa uwezeshaji laleta matumaini kwa wanawake wajane Afrika

Wanawake wajane kote barani Afrika wamepata matumaini mapya baada ya kutolewa pendekezo la kudhaminiwa fedha za kuwawezesha kimaisha. Mpango huo umependekezwa na mke wa Naibu Rais wa Kenya, Bi Dorcas Rigathi, wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Wajane wa Afrika uliofanyika Zanzibar.

Fedha za mpango huo zinalenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazokabili mamilioni ya wanawake wajane barani Afrika.

Mfuko wa Uwezeshaji wa Wajane barani Afrika utaanza kwa kufadhiliwa kwa ruzuku ya Naira milioni 10 sarafu ya Nigeria sawa na dola 27,300 za Kimarekani iliyotolewa na Abdul Samad Rabiu Initiative for Africa (ASR Africa). Katika siku za usoni, serikali za Afrika zitachangia mfuko huo ili kuhakikisha unaendelea, unastawi na unatanua wigo wa huduma zake kwa wajane zaidi katika bara zima la Afrika.

David Matinde kutoka Mathare Light Centre ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linalojitolea kuinua hali ya wanawake katika vitongoji duni vya Mathare jijini Nairobi kupitia kukuza ujuzi wao, kuwapa mafunzo, ushauri na kuwaonesha njia za kuwawezesha kiuchumi, amepongeza mpango huo.

Bi Mary Kamau, mkulima mwenye umri wa miaka 52 kutoka Kiambu, ambaye amekuwa akisimamia shamba dogo ili kulisha familia yake, ni miongoni mwa wanawake wengi wajane waliotoa mawazo yao kuhusu pendekezo hilo.

Amesema: "Mpango huu utabadilisha maisha. Ina maana kwamba hatimaye tunaweza kuwa na rasilimali za kuboresha mbinu zetu za kilimo na kuongeza tija."

Mkutano huo wa kilele uliofanyika mwezi uliopita mjini Unguja huko Zanzibar uliwaleta pamoja wanawake wajane zaidi ya 800 kutoka mataifa mbalimali ya Afrika, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Cameroon, Tanzania, Kenya na Zimbabwe. 

Tags