Magaidi 80 wa al-Shabaab waangamizwa na jeshi la Somalia
Makumi ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa nchini Somalia katika operesheni tatu za jeshi la Somalia dhidi ya genge hilo.
Hayo yameripotiwa na Wizara ya Habari ya Somalia ambayo imeeleza kuwa, Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) kwa ushirikiano na vikosi vya kieneo vya jimbo la Jubaland mapema leo Jumatatu limefanikiwa kuzima operesheni za al-Shabaab katika medani tatu za vita huko Magharibi na Kusini mwa Kismayo, makao makuu ya kiutawala ya Jubaland.
Inaarifiwa kuwa, mapema leo, wanachama wa al-Shabaab walivamia eneo la Harbole karibu na kijiji cha Mido, magharibi mwa Kismayo, lililotokewa na al-Shabaab siku 12 zilizopita. Hata hivyo wanajeshi wa Somalia wamefanikiwa kulidhibiti tena eneo hilo baada ya kuwapa vipigo wapiganaji wa al-Shabaab.
Kadhalika genge hilo la kigaidi limepata vipigo vikali mapema leo pia kutoka Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) na vikosi vya jimbo la Jubaland, katika mji wa Bula Haji, yapata kilomita 90 kusini mwa Kismayo.
Genge la kigaidi la al-Shabaab linaonekana kupunguza mashambulizi yake tangu Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud kutangaza "vita vya kila namna" dhidi ya genge hilo.
Kampeni hiyo inaonekana imefanikiwa kiasi kwamba, hivi sasa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kinaendelea na mchakato wa kuondoa askari wake nchini humo ili kukabidhi masuala yote ya ulinzi kwa vikosi vya serikali ya Somalia.