UN: Magaidi wa ISIS yamkini wakaenea Afrika baada ya kushindwa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11566-un_magaidi_wa_isis_yamkini_wakaenea_afrika_baada_ya_kushindwa_libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa magaidi wa kundi la ISIS au Daesh yamkini wakaenea maeneo mengine barani Afrika baada ya kupata pigo kubwa katika mji wa Sirte nchini Libya, ambayo ilikuwa ngome yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2016 09:16 UTC
  • Ban Ki-moon
    Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa magaidi wa kundi la ISIS au Daesh yamkini wakaenea maeneo mengine barani Afrika baada ya kupata pigo kubwa katika mji wa Sirte nchini Libya, ambayo ilikuwa ngome yao.

Katika ripoti ya siri kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban amesema mafanikio ya hivi karibuni ya jeshi la Libya dhidi ya ISIS ni jambo ambalo limeibua wasiwasi kuwa yamkini magaidi hao , wakahama na kujikusanya katika makundi madogo madogo katika maeneo mengine ya Libya na hata nchi zingine za Kiafrika.

Amesema tayari magaidi wengi wa ISIS wameshatoroka Libya na kukimbilia katika nchi jirani ya Tunisia.

Magaidi wa ISIS wakiwa Sirte, Libya

 

Mji wa Sirte, ulitekwa na magaidi wa ISIS Februari mwaka 2015 na kubadilika kuwa ngome kubwa zaidi ya kundi hilo la kigaidi  barani Afrika.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuna magaidi 2,000 hadi 5,000 wa ISIS nchini Libya na aghalabu ni raia wa Libya, Algeria, Egypt, Mali, Morocco na Mauritania.

Magaidi wa ISIS wameweza kujipeneyza Libya kutokana na mapigano ya ndani yaliyojiri nchini humo baada ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kuongoza mapinduzi yaliyomuangusha dikteta wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011.