Sep 05, 2024 12:44 UTC
  • Mwanariadha wa Uganda auawa kwa kuchomwa moto

Madaktari na maafisa wa riadha wametangaza kuwa, mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei, aliyeshiriki katika michezo ya Olimpiki nchini Ufaransa amefariki dunia nchini Kenya leo.

Siku nne zilizopita mwanariadha huyo alichomwa moto na mpenzi wake.

Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Uganda, Donald Rukare, amesema kwenye mtandao wa X kwamba tukio hilo la mwanariadha Cheptegei kuuliwa na mpenzi wake ni la unyanyasaji wa kijinsia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki,  huku wanaharakati wakitahadharisha kuhusu janga la mauaji ya wanawake.

Kulingana na polisi ya Kenya, mwanamume anayetambuliwa kama mpenzi wa Cheptegei anayeitwa Dickson Ndiema Marangach, alimmwagia petroli na kumchoma msichana huyo siku ya Jumapili nyumbani kwake Endebess katika kaunti ya Trans-Nzoia, magharibi mwa Kenya.

Mzee Joseph Cheptegei, babake marehemu mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei ameelezea masikitiko makubwa kwa kumpoteza binti yake huku akitaka haki itendeke.

Rebecca Cheptegei

 

Cheptegei ambaye alikuwa akihutubia wanahabari katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret muda mfupi baada ya kupokea habari hizo alisema kuwa familia hiyo sio tu imempoteza binti mpendwa bali pia mlezi.

Wakati huo huo, waziri wa michezo nchini Kenya, Kipchumba Murkomen amemuomboleza mshikilizi wa Rekodi ya Wanawake Marathon Rebecca Cheptegei, akisema kifo chake ni hasara kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Murkomen katika taarifa aliotoa siku ya Alhamisi alisema kifo chake ni ukumbusho kwamba juhudi zaidi zinafaa kuwekwa ili kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

Marehemu Cheptegei anasemekana alipata asilimia 80 ya majeraha ya moto baada ya anayedaiwa kuwa mpenzi wake kumwagia mafuta ya petroli mwilini mwake na kumchoma moto.

Tags