Ukame waendelea kuizonga Madagascar
Serikali ya Madagascar imeendelea kukumbwa na mgogoro wa ukosefu wa chakula kutokana na hali ya ukame na ungezeko la jangwa ndani ya nchi hiyo.
Ripoti zinasema tangu mwezi Februari mwaka huu, viongozi wa serikali ya Antananarivo walianza kutekeleza hatua za kukabiliana na utapiamlo na uhaba wa chakula hususan katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Hata hivyo changamoto hiyo imeendelea kushuhudiwa nchini na hivyo kuzidisha hali ya wasiwasi. Ukame na kuongezeka kwa jangwa, mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na El Nino, matatizo ya kutopatikana kwa maji na kukosekana kwa miundombinu inayotosha kwa ajili ya kustawisha kilimo ni mambo ambayo yameizidishia matatizo makubwa serikali ya Rais Hery Rajaonarimampianina.
Inaelezwa kuwa tayari serikali imechukua hatua za kuhuisha sekta ya kilimo ambapo mwezi Septemba mwaka huu itatoa ripoti kamili kuhusiana na suala hilo. Zaidi ya watu milioni mbili wanakabiliwa na utapiamlo nchini Madagascar kutokana na kukosekana chakula.