Polisi ya Kenya 'yasutwa' kwa kudai hakuna Wakenya waliotekwa nyara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120662-polisi_ya_kenya_'yasutwa'_kwa_kudai_hakuna_wakenya_waliotekwa_nyara
Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imekanusha ripoti ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kwamba hakuna Wakenya waliotekwa nyara nchini humo ikisema, katika mwezi huu wa Desemba pekee, watu saba hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wametekwa nyara; na kufikia sasa, sita hawajulikani waliko.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 27, 2024 03:54 UTC
  • Polisi ya Kenya 'yasutwa' kwa kudai hakuna Wakenya waliotekwa nyara

Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imekanusha ripoti ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kwamba hakuna Wakenya waliotekwa nyara nchini humo ikisema, katika mwezi huu wa Desemba pekee, watu saba hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wametekwa nyara; na kufikia sasa, sita hawajulikani waliko.

Mwenyekiti wa KNCHR Rosylene Odede amesema tume yao inaendelea kufuatilia mtindo unaotia wasiwasi wa utekaji nyara katika maeneo kadhaa ya Kenya.

Odede ameeleza katika taarifa: “tume imebainisha kuwa utekaji nyara huu unaendelezwa kwa siri na watu wasiojulikana wakiwa na silaha. Tume inabainisha zaidi kwamba waliotekwa nyara wamekuwa wakosoaji (serikali), hasa kwenye mitandao ya kijamii”.

Amefafanua kuwa, kumekuwepo na matukio kumi na tatu zaidi ya utekaji nyara au kutoweka kwa watu katika kipindi cha miezi mitatu na kufanya jumla ya visa vya utekaji nyara kuwa 82 kuanzia Juni 2024 hadi sasa.

Taarifa ya KNCHR imesisitiza kwa kusema: “tume, inalaani vikali utekaji nyara huu ambao uko nje ya Katiba. Utekaji nyara ni mateso, ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa binadamu. Hauna nafasi katika nchi ya kidemokrasia kama yetu! Tume inatahadharisha kwamba ikiwa mtindo huu wa utekaji nyara utaendelea, basi tutakuwa tunarejea kwa kasi katika siku za giza za historia yetu ambapo matukio kama hayo yalikuwa yanaleta hofu kwa mtu yeyote anayeikosoa Serikali.”

Aidha Bi Odede amesema, tume hiyo ina wasiwasi kuhusu taarifa iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi Desemba 26, 2024, ikisema kwamba Polisi hawahusiki na utekaji nyara huo.

Mwenyekiti wa KNCHR amekumbusha kuhusu jukumu lililonalo jeshi la Polisi la kumlinda kila mtu nchini Kenya na vitendo hivyo vya kikatili hasa kutokana na kubainika kuwa vitendo vya utekaji nyara vinafanyika mchana kweupe, huku baadhi ya wanaohusika wakinaswa kwenye CCTV lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.../