Sudan: Vyombo vya habari vya Magharibi vinapotosha ukweli kuhusu vita
Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan amevituhumu vyombo vya habari vya Magharibi kwa kupotosha uhakika wa mambo kuhusiana na vita vinavyoendelea nchini humo akisema kuwa vyombo hivyo vinaegemea upande wa kikosi cha RSF.
Sudan ilitumbukia katika hali ya amchafuko mwezi Aprili mwaka jana huku mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi na kikosi cha msaada wa haraka (RSF) ukiibua vita nchini humo.
Tokea wakati huo hadi sasa, mamilioni ya wananchi wa Sudan wamelazimika kuhama makazi yao huku maelfu ya wengine wakiuawa vitani.
Khalid Alesir Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan amevituhumu vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuwa vinaegemea upande wa kikosi cha RSF kuhusiana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi ya Sudan na kundi hilo la wanamgambo.

Amesema vyombo vya habari vya Magharibi vinalituhumu jeshi la Sudan kuwa linawashambulia raia na kusema kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote.
"Waulize watu wa Sudan, je wanadhani kwamba jeshi linatekeleza mashambulizi dhidi yao; jibu litakuwa jeshi la Sudan haliwalengi raia,"amesema Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan.
Amesema kuwa, wanamgambo wa RSF wanatekeleza mashambulizi dhidi ya raia, vitendo vya ubakaji, uporaji na kuwafukuza raia katika makazi yao huku jeshi la Sudan likiwalinda watu wanaokimbia kutoka katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa RSF.