Chad yakosoa ubabe na ukoloni wa Ufaransa
Kufuatia kauli za Rais wa Ufaransa kwamba nchi za Afrika zimesahau kuishukuru Paris kwa kushiriki katika kile anachosema ni 'mapambano dhidi ya ugaidi' katika eneo la Sahel, Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad amekosoa maneno hayo na kuyalaani.
Abdulrahman Ghulamallah, akieleza wasiwasi wa serikali ya Jamhuri ya Chad kuhusu matamshi ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kuwa matamshi hayo ni aina ya mtazamo wa kudharau Afrika na Waafrika. Amesisitiza kuwa viongozi wa Ufaransa wanapaswa kuelewa umuhimu wa kuheshimu watu wa Afrika.
Viongozi wa Paris wamekasirishwa na mwelekeo mpya wa nchi za Afrika. Kwa miongo kadhaa, Wafaransa walizikalia kwa mabavu nchi mbalimbali za Afrika bila mipaka, wakizitumia kama uwanja wa uporaji maliasili. Katika vipindi mbalimbali vya historia, waliendeleza ukoloni wa zamani na pia ukoloni mamboleo, na katika miongo ya hivi karibuni walihalalisha uwepo wao barani Afrika kwa kisingizio cha msaada na ushirikiano.

Kwa hakika, Ufaransa imekuwa ikichukulia Afrika kama sehemu ya kutekeleza sera zake za kujitanua kibeberu katika uga wa kimataifa. Katika kujitanua huko katika miongo ya karibuni, Ufaransa imekuwa ikipora rasilimali na mali za Afrika.
Hoja ya kusaidia nchi za Afrika kupambana na ugaidi na kuhakikisha usalama, ni moja ya mada ambazo mara kwa mara viongozi wa Ufaransa wamekuwa wakizitumia kutetea uwepo wao wa kijeshi barani humo. Jeshi la Ufaransa limekuwa likihudumu katika nchi za Sahel kama Mali, Burkina Faso na Niger, si kwa maslahi ya usalama bali kwa lengo la kuingilia masuala ya kisiasa na kulazimisha sera zinazowanufaisha wao wenyewe.
Kuendelea kwa sera za uingiliaji kati wa Ufaransa katika nchi za Afrika, sambamba na mabadiliko ya kisiasa na kijamii katika mataifa mengi ya bara hilo, kumewafanya watu wa Afrika wapinge siasa za kikoloni za mataifa ya Magharibi, ikiwemo Ufaransa. Katika miaka ya hivi karibuni, mapinduzi kadhaa ya kijeshi yanayoungwa mkono na wananchi yamefanyika Mali, Niger na Burkina Faso ambapo raia walionyesha wazi kuunga mkono kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa kwenye nchi zao.
Hali hii inaonyesha mwisho wa ukoloni mamboleo wa Ufaransa barani Afrika na mwanzo wa enzi mpya ya uhuru wa kisiasa na kiuchumi wa mataifa mbalimbali ya Afrika.
Kwa mtazamo wa mataifa mengi ya Afrika, Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi sasa haziwezi tena kuendelea kuweka majeshi au kupora rasilimali za na rasilimali za madini ya mataifa ya Afrika. Badala yake, zinapaswa kukubali uhusiano mpya unaojengwa juu ya kuheshimiana. Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad amesisitiza: "Ufaransa sasa inapaswa kuelewa kuwa Chad imekua na imepevuka."
Hata hivyo, viongozi wa Paris, ambao katika miaka ya hivi karibuni wamelazimika kukubali kushindwa na kuondoa majeshi yao katika mataifa mbalimbali ya Afrika, sasa katika mkakati mpya wanataka mataifa ya Afrika yatambue mchango wa Paris katika kile wanachodai ni vita dhidi ya ugaidi, huku wakiwaita Waafrika kuwa watu wasio na shukrani. Kauli hiyo imemfanya Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad, Abdulrahman Ghulamullah, kujibu kwa kusema kuwa ushiriki wa Ufaransa kwa kipindi cha miaka sitini ulijikita kwa manufaa ya kisiasa ya Ufaransa pekee bila kuwa na mchango halisi wa maendeleo endelevu barani Afrika.

Viongozi wa Ufaransa pia wanataka kutambuliwa kutoka kwa nchi za Afrika, huku wakiwa hawajawahi kuomba msamaha kwa uhalifu wao barani Afrika. Rekodi za mauaji na ukatili wa Ufaransa huko Algeria, Rwanda, Cameroon, na mataifa mengine zinasalia kuwa sehemu ya historia, na licha ya maombi ya mara kwa mara ya mataifa haya, hasa Algeria, Ufaransa imekataa kuomba radhi rasmi.
Jambo lingine ni kwamba Ufaransa haijawahi kutambua mchango wa Afrika katika mafanikio yake kiuchumi na kisiasa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad amesema kuwa Afrika ilikuwa na mchango muhimu katika ukombozi wa Ufaransa katika Vita Kuu Mbili za Dunia. Amesema Ufaransa haijawahi kwa dhati kuthamini kujitolea kwa wanajeshi wa Kiafrika.
Kwa msingi huo si ti kwamba Ufaransa inapaswa kuzishukuru nchi za Afrika kwa kuisaidia, bali pia inapaswa kuomba msamaha na kulipa fidia kutokana na jinai ambazo ilitenda dhidi ya Waafrika katika zama za ukoloni.