China yaiambia G20: Lazima dunia iisikilize Afrika, iyape uzito masuala yanayoitia wasiwasi
Feb 22, 2025 05:55 UTC
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema, lazima dunia isikilize "kile Afrika inachosema" na kuuchukulia wasiwasi ilionao Afrika "kwa uzito". Wang ameyasema hayo katika hotuba yake mbele ya hadhara ya washiriki wa mkutano wa Kundi la Mataifa 20 (G20) unaofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
"Lazima tusikilize kile Afŕika inachosema, tuupe uzito wasiwasi ilionao Afrika, tuunge mkono hatua za Afŕika, na kufanyia kazi amani na maendeleo baŕani Afŕika, ili kuacha alama ya kipekee ya Kiafŕika katika Mkutano wa Kilele wa Johannesburg,”amesisitiza waziri huyo wa mambo ya nje wa China alipohutubia mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa G20 katika mji mkuu huo wa Afŕika Kusini.
Kwa sasa Afrika Kusini ndiyo inayoshikilia wadhifa wa urais wa G20 ulioanza Disemba mwaka jana hadi Novemba mwaka huu.
Mkutano huo wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje ulikuwa wa kwanza wa kilele wa G20 kuandaliwa na mji wowote wa Afrika kwani Afrika Kusini ndiyo nchi pekee ya Afrika mwanachama wa kundi hilo, ambalo linajumuisha pia nchi za Umoja wa Ulaya.
Mwaka jana, Umoja wa Afrika uliongezwa kwenye G20 kama mwanachama wa 21.
"Mwaka huu unawakilisha 'wakati wa Afrika'," ameeleza Wang akitilia mkazo pia "uungaji mkono" wa Beijing kwa watu wa Afrika "kutatua matatizo ya Afrika bila ya kuingiliwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameeleza bayana kuwa Beijing "inapinga" uingiliaji kati wa nje katika masuala ya ndani ya nchi za Afrika.../
Tags