Waziri mashuhuri wa upande wa upinzani Sudan Kusini ajiuzulu
Waziri mashuhuri wa serikali ya Sudan Kusini kutoka upande wa upinzani amejiuzulu wadhifa wake, hatua iliyotajwa kuwa ni pigo kubwa kwa makubaliano ya amani yanayolegalega ya nchi hiyo.
Akizungumza leo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Addis Ababa Ethiopia, Lam Akol Ajawin aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Sudan Kusini amemlaumu Rais Salva Kiir kuwa amedhoofisha makubaliano ya amani kwa kudaiwa kuongoza shambulio la kijeshi dhidi ya Makamu wa zamani wa Rais Riek Machar. Waziri huyo aliyejiuzulu amemtuhumu Rais Kiir kuwa amemuondoa kwa nguvu Machar huko Juba na badala yake kuijaza nafasi yake kwa kumteuwa shakhsia anayemtaka.
Lam Akol Ajawin amesema hakuna makubaliano yoyote ya amani yanayohitaji kutekelezwa huko Juba. Amesema njia pekee ya busara ya kuupinga utawala wa Juba ili kuweza kurejesha amani ya kudumu huko Sudan Kusini ni kujipanga nje ya Juba. Ajawin ameandika barua ya kujiuzulu inayoeleza kuwa, mtu hawezi kwa moyo safi kufanya kazi katika serikali kama hiyo ya Sudan Kusini.