Kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo huko Sudan Kusini
Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hali ya mambo katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba imezidi kuwa mbaya.
Ramlan bin Ibrahim mwanadiplomasia wa Malaysia na mwenyeikuiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Agosti amesisitiza kuwa, ujumbe maalumu wa baraza hilo unakusudia kufanya safari katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ili sanjari na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo, ufanye juhudi za kusitisha mapigano na kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Duru za habari zinasema kuwa, yamkini safari ya ujumbe huo wa Baraza la Usalama ikafanyika tarehe 15 ya mwezi huu.
Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kuongeza muda wa kuhudumu huko Sudan Kusini vikosi vya kimataifa vya kusimamia amani.
Vikosi hivyo vipo katika maeneo mbalimbali ya Sudan Kusini na jukumu lao kuu ni kulinda roho na uhai wa raia wa nchi hiyo.
Muda wa kuhudumu vikosi hivyo umeongezwa ili wanadiplomasia wapate muda wa kutosha wa kufanya mazungumzo kuhusiana na vikwazo vya silaha na kupata idhini ya kutumwa vikosi vya kieneo huko Juba.
Viongozi wa nchi za Kiafrika katika Umoja wa Afrika juma lililopita waliafikiana kutuma kikosi maalumu katika mji wa Juba. Hata hivyo mwafaka huo unapaswa kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, Waziri wa Kilimo wa Sudan Kusini amejiuzulu wadhifa wake huo akilalamikia kile alichokieleza kuwa, kutotekelezwa vipengee vya mkataba wa amani wa Sudan Kusini. Lam Akol Ajawin anaamini kwamba, mkataba wa amani wa Sudan Kusini umekufa hivyo hata Salva Kiir, Rais wa serikali ya umoja wa kitaifa naye anapaswa kuachia ngazi.
Lam Akol ambaye ni mjumbe katika chama cha upinzani cha Sudan People's Liberation Movement - Democratic Change amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Addis Ababa Ethiopia. Amesisitiza kuwa, mirengo na vyama vyote vya Sudan Kusini vinaafikiana kwa kauli moja kwamba, utawala wa nchi hiyo unapaswa kubadilishwa.
Katika uchaguzi wa kieneo wa mwaka 2010 Lam Akol alikuwa akihesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Salva Kiir. Uchaguzi huo ulifanyika katika hali ambayo, Sudan Kusini ilikuwa na mamlaka ya ndani na mwaka uliofuata ikajipatia mamlaka kamili.
Aidha Lam Akol ni mmoja wa wapinzani wa Riek Machar makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini. Kwa mujibu wa makubaliano ya Agosti mwaka jana, baada ya kumalizika machafuko, Machar aliteuliwa tena kuwa Makamu wa Rais na kisha ikaundwa serikali ya umoja wa kitaifa iliyokuwa na mawaziri takribani 30. Nyadhifa za wizara ziligawanywa baina ya mirengo miwili mikuu na vyama vingine vya nchi hiyo.
Baada ya hapo Riek Machar alirejea Juba; lakini mwanzoni mwa mwezi uliopita kwa mara nyingine tena kukaibuka machafuko ya umwagaji damu baina ya vikosi vitiifu kwa Machar na vile vya Rais Salva Kiir. Kufuatia machafuko hayo, Machar akaondoka tena Juba. Wiki iliyopita Salva Kiir alimteua Taban Deng Gai kujaza nafasi ya Riek Machar.
Wachambuzi wa mambo wana wasiwasi mkubwa na mwenendo wa utekelezwaji hati ya makubaliano ya amani ya Sudan Kusini pamoja na kuendelea kulegalega hali ya mambo na mgogoro wa nchi hiyo. Katika mazingira kama haya ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mtaifa una matumaini kwamba, hali ya usalama ya Sudan Kusini itaupa mwanya wa kusafiri na kuelekea Juba kwa ajili ya kuzishajiisha pande mbili zitekeleze hati ya makubaliano ya amani.