Somalia yazindua mpango wa chanjo nchi nzima ili kukabiliana na surua, polio na nimonia
Somalia leo Jumatatu imezindua kampeni ya chanjo ya kitaifa ili kukabiliana na magonjwa ya surua, polio na nimonia. Kampeni hiyo ya chanjo imekusudia kuwafikia watoto zaidi ya milioni 3 nchini humo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo limezindua kampeni hiyo ya wiki moja kwa kushirikiana na serikali kuu na za majimbo za Somalia imeeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ya utoaji chanjo ni kuwalinda na magonjwa hatari yanayoweza kuzuilika watoto na jamii zilizo katika mazingira hatarishi katika eneo la Pembe ya Afrika.
Muungano wa Chanjo wa Kimataifa (GAVI) unafadhili kampeni hiyo iliyoazimia kutoa chanjo kwa watoto wa Kisomali milioni tatu na laki moja walio na umri wa chini ya miaka mitano dhidi ya magonjwa ya surua, poliso na nimonia.
Somalia inaendelea kuathiriwa na changamoto za kiusalama za muda mrefu na hivyo kutatiza zoezi la utoaji chanjo kwa watoto wenye mahitaji nchini humo.
Tangu 2014, hakuna virusi vya polio vilivyogunduliwa nchini Somalia, na mwaka 2020 bara la Afrika lilitangazwa kutokuwa na virusi hivyo.
Hata hivyo ripoti za WHO zinasema kuwa miundombinu ya kiafya ya Somalia imeharibiwa na machafuko, umaskini na matatizo ya mabadiliko ya tabianchi na kwamba ugonjwa wa polio unaendelea kutishia maisha ya watoto.