AU yalaani shambulio dhidi ya msafara wa Rais wa Somalia
(last modified Thu, 20 Mar 2025 03:11:23 GMT )
Mar 20, 2025 03:11 UTC
  • AU yalaani shambulio dhidi ya msafara wa Rais wa Somalia

Somalia na Umoja wa Afrika (AU) zimelaani shambulizi la kigaidi lililolenga msafara wa Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud huko Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika taarifa tofauti, Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii ya Somalia na Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, wamelaani shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari kwenye msafara huo wakati rais alipokuwa akisafiri kuelekea kwenye mstari wa mbele wa medani ya vita katikati mwa Somalia, ili kuendeleza mapambano dhidi ya al-Shabaab.

Wizara hiyo imeeleza bayana kuwa, raia wasio na hatia waliuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea Jumanne asubuhi.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU amesema katika taarifa kuwa: Kitendo hiki cha kuchukiza cha ugaidi, kilichofanyika kwenye makutano yenye shughuli nyingi katika mji mkuu, ni jaribio jingine la kukata tamaa la al-Shabaab kudhoofisha azimio la watu wa Somalia na uongozi.

Youssouf ametoa wito wa kuwepo kwa umakini na kuendelea kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuushinda ugaidi, na kurejesha amani na utulivu wa kudumu nchini Somalia na eneo pana la Pembe ya Afrika.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud aliyenusurika kuuawa

Serikali ya Somalia imetangaza kuwa mlipuko uliotokea Jumanne mjini Mogadishu ulikuwa jaribio la kumuua rais wa nchi hiyo, ambalo limetekelezwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab. 

Wizara ya Habari ilisema msafara wa Rais Hassan Sheikh Mohamud ulikabiliwa na shambulio karibu saa nne na nusu asubuhi katika wilaya ya Xamar-Jajab mjini Mogadishu.