WFP yaonya juu ya kupungua msaada wa chakula kwa wakimbizi Kenya
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) jana Alkhamisi lilionya kwamba, wakimbizi nchini Kenya wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa huku uhaba mkubwa wa fedha ukilazimisha shirika hilo kupunguza msaada wa chakula hadi viwango vya chini zaidi.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema linahitaji haraka dola milioni 44 za Marekani kutoa mgao kamili na kurejesha msaada wa fedha taslimu kwa wakimbizi 720,000 hadi mwezi Agosti. Bila fedha za ziada, mgao wa chakula utapunguzwa hadi asilimia 28 tu ya mahitaji ya kila siku mwezi Juni, na usaidizi wote wa pesa pia utasitishwa.
Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya, Bai Mankay Sankoh alisema katika taarifa yake aliyoitoa Nairobi, mji mkuu wa Kenya kwamba, shughuli za shirika hilo linalosaidia wakimbizi nchini Kenya zinakabiliwa na matatizo makubwa.
"Usaidizi mdogo utawalazimu wakimbizi kufanya maamuzi ya kuhuzunisha, kuuza mali na bidhaa zao muhimu, kuwaondoa watoto shuleni, au hata kurejea katika nchi zao licha ya hatari," Sankoh amesema.

Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya ameongeza kuwa, "Msaada wa chakula ni kiungo muhimu cha usalama, na tutaendelea kujitolea kufanya kila tuwezalo kuwasaidia wakimbizi ambao wanajaribu kujenga upya maisha yao kwa usalama."
Idadi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Kenya imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kuongezeka kutoka karibu 500,000 hadi 843,000, huku mizozo na majanga ya hali ya hewa yakiendelea kusababisha watu kuhama kutoka nchi jirani kama vile Somalia na Sudan Kusini, WFP imesema.