Kabila: Mfumo wa sheria wa DRC unavunda
(last modified Sat, 24 May 2025 07:47:53 GMT )
May 24, 2025 07:47 UTC
  • Kabila: Mfumo wa sheria wa DRC unavunda

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila jana Ijumaa ameshutumu vikali mfumo wa sheria wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati, akisema kuwa umeoza kutokana na uendeshaji mbaya.

Kabla amesema hayo saa chache baada ya Bunge la Seneti la nchi hiyo kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, na kufungua njia ya mwanasiasa huyo kufunguliwa mashtaka.

"Kuhusu mfumo wa haki, umeachana kabisa na majukumu yake, na kuruhusu kupindishwa kwa malengo ya kisiasa," Kabila, ambaye amekanusha kuwa na uhusiano wowote na kundi la waasi la M23, alisema hayo katika hotuba yake Ijumaa jioni.

"Kwa hivyo sio kitu zaidi ya chombo cha ukandamizaji kwa udikteta unaojaribu sana kubakia hai," amesisitiza Kabila ambaye pia ni seneta wa maisha. Kadhalika alitoa wito wa kuondolewa mara moja kwa wanajeshi wote wa kigeni katika ardhi ya taifa hilo.

Kabila anatuhumiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, na kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo liliteka miji mikubwa Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.

Anakuwa Mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi kushtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita na mashtaka yanayohusiana nayo. Uamuzi huo sasa unatoa nafasi kwa mahakama ya kijeshi kuanzisha kesi dhidi yake.

Mwezi uliopita, Waziri wa Sheria alipeleka suala hilo kwenye mahakama za kijeshi ili kuanzisha kesi dhidi ya mkuu huyo wa zamani wa nchi "kwa ushiriki wake wa moja kwa moja" katika vuguvugu la M23 katika muktadha wa kushadidi mzozo mashariki mwa DRC.