Mufti Mkuu wa zamani wa Misri anusurika jaribio la mauaji
Vyombo vya usalama nchini Misri vimesema Mufti Mkuu wa zamani wa Misri na mwanachuoni mkubwa wa nchi hiyo ambaye amekuwa akikosoa makundi ya kigaidi na kitakfiri ameponea chupuchupu kuuawa katika jaribio la mauaji dhidi yake hii leo.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, Sheikh Ali Gomaa, aliyekuwa Mufti Mkuu wa Misri ameponea chupuchupu katika jaribio la mauaji baada ya watu wawili waliokuwa juu ya pikipiki kumfyatulia risasi alipokuwa akielekea msikitini mjini Cairo. Hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na jaribio hilo la mauaji.
Mufti huyo aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, Uwahabbi na Usalafi hauna chochote isipokuwa ni ugaidi na misimamo ya kufurutu ada. Mwanachuoni huyo wa ngazi za juu wa Misri alisema makundi hayo ya kufurutu ada hayana mizizi katika Uislamu na kwamba Usalafi si madhehebu bali ni kundi la watu wanaoendeleza harakati za kimaslahi.
Aidha inaarifiwa kuwa msomi huyo ni mpambe wa karibu wa Rais Abdul Fattah el-Sisi wa nchi hiyo, aliyeongoza mapinduzi ya kumuondoa madarakani rais wa kwanza kuchaguliwa kwa misingi ya nchini humo demokrasia Mohamed Mursi mwaka 2013.
Jaribio hilo la mauaji dhidi ya mwanachuoni huyo wa Misri limejiri siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kutangaza kuwa limemuangamiza kamanda mkuu wa kundi la kigaidi la Daesh katika Peninsula ya Sinai.
Habari zinasema kuwa, Abu Duaa al-Ansari aliuawa pamoja na makumi ya wanachama wa kundi hilo la kitakfiri katika mashambulizi ya anga katika eneo la Sinai.