Rasmi; Rais wa Cameroon, Paul Biya (92) kugombea muhula mwingine katika uchaguzi ujao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128318
Rais wa sasa wa Cameroon, Paul Biya ametangaza kuwa atagombea muhula wa nane katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Oktoba 12, na hivyo kuhitimisha uvumi wa miezi kadhaa wa iwapo atawania au la.
(last modified 2025-07-15T05:05:40+00:00 )
Jul 14, 2025 12:56 UTC
  • Rasmi; Rais wa Cameroon, Paul Biya (92) kugombea muhula mwingine katika uchaguzi ujao

Rais wa sasa wa Cameroon, Paul Biya ametangaza kuwa atagombea muhula wa nane katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Oktoba 12, na hivyo kuhitimisha uvumi wa miezi kadhaa wa iwapo atawania au la.

Biya, 92, kiongozi wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani, aliingia madarakani mwaka wa 1982. Hata hivyo, katika taarifa yake, Biya amesema ingawaje matokeo ya utawala wake wa muda mrefu yanaonekana na kusifiwa, bado kuna mengi ya kufanywa.

"Katika kukabiliana na mazingira magumu ya kimataifa yanayozidi kuwa magumu, changamoto zinazotukabili ni kubwa zaidi na zaidi. Katika hali kama hiyo, siwezi kukwepa dhamira yangu," amesema. Amebainisha kuwa, azma yake ya kuwatumikia wananchi wa Cameroon inatokana na changamoto kubwa zinazowakabili.

Amefafanua zaidi kwa kusema, "Kwa hivyo nimeamua kutii miito mingi na wa kusisitiza kutoka mikoa 10 ya nchi yetu na kutoka kwa diaspora (nje ya nchi). Mimi ni mgombea wa uchaguzi wa rais wa tarehe 12 Oktoba 2025."

Mwaka 2018, Biya alishinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura, ingawa uchaguzi huo ulikumbwa na dosari nyingi na kiwango cha chini cha ushiriki kutokana na mashambulizi ya waasi wa makundi yanayotaka kujitenga na makundi ya kigaidi.

Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.

Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa uchaguzi wa urais utafanyika tarehe 12 Oktoba. Hayo ni kwa mujibu wa amri iliyosainiwa Ijumaa na Rais Paul Biya mwenyewe.