Wahamiaji 7 wa Ethiopia wameaga dunia kwa njaa na kiu wakielekea Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129274-wahamiaji_7_wa_ethiopia_wameaga_dunia_kwa_njaa_na_kiu_wakielekea_yemen
Wahamiaji saba wa Ethiopia wameaga dunia kutokana na njaa na kiu baada ya boti waliyokuwa wakisafiri kuharibika njiani wakitoka Somalia kuelekea Yemen.
(last modified 2025-08-08T02:37:56+00:00 )
Aug 08, 2025 02:37 UTC
  • Wahamiaji 7 wa Ethiopia wameaga dunia kwa njaa na kiu wakielekea Yemen

Wahamiaji saba wa Ethiopia wameaga dunia kutokana na njaa na kiu baada ya boti waliyokuwa wakisafiri kuharibika njiani wakitoka Somalia kuelekea Yemen.

 Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema katika taarifa yake kuwa, timu ya  wafanyakazi wa shirika hilo huko Yemen imewapatia msaada watu walionusurika baada ya mashua yao kuharibika.

Shirika la IOM limeongeza kuwa, boti iliyokuwa imebeba wahamiaji 250 wa Ethiopia wakiwemo watoto 82 iliwasili katika eneo la Arqah kusini mwa Yemen Jumanne wiki hii na kwamba wahamiaji saba wameaga dunia kwa njaa na kiu wakiwa njiani. 

Abdulsattor Esoev Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Yemen ameeleza kuwa wahamiaji hao wa Kiethiopia walipitia hali ngumu wakiwa katika bahari kuu kwa muda wa wiki moja ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa na kutishwa. 

Tangu kuanza mwaka huu wa 2025, shirika la IOM limeripoti visa vya kuaga dunia wahamiaji 350 wakiwa safarini baharini. 

mapema wiki hii zaidi ya wahamiaji 50 walifariki dunia na wengine kutoweka baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji wa Kiafrika kuzama katika Bahari ya Arabia kwenye pwani ya Yemen.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa afya katika Wilaya ya Zinjibar, Jimbo la Abyan, miili 54 ya wahamiaji wa kiume na wa kike imeopolewa, huku wengine 10 wakiokolewa, wakiwemo raia tisa wa Ethiopia na mmoja wa Yemen.

Wahajiri hawa ambao wengi wao wanatoka Ethiopia na Somalia, mara nyingi hukimbia kutokana na hali ngumu ya maisha kupitia njia inayoitwa njia ya Mashariki, ambayo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linaitaja kuwa mojawapo ya korido zenye shughuli nyingi na hatari zaidi za wahamiaji duniani.‏