Aug 17, 2016 04:18 UTC
  • Maelfu ya wanawake wamebakwa kwenye migodi Afrika Kusini

Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka MSF limetoa ripoti inayoonyesha kutokea visa vingi vya ubakaji katika eneo la migodi la Rustenburg nchini Afrika Kusini

Taarifa ya shirika hilo inasema kuwa,  katika manispaa ya Rustenberg mwanammke mmoja kati ya wanne wamewahi kubakwa.

Kwa mujibu wa madaktari wa MSF kiasi ya wanawake elfu hamsini na wasichana kutoka watu laki mbili na nusu wanaoishi Rustenburg, wamebakwa.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba, ni asilimia tano tu kati ya wanawake hao waliobakwa ambao waliripoti mikasa iliyowapata

Utafiti wa hivi karibuni unaashiria kuwa idadi ndogo ya wanawake hawa walitambua namna ya kuepuka kuambukizwa virusi vya ugonjwa hatari wa ukimwi na hata pia kushika mimba baada ya kubakwa.

Licha ya kuwa mji wa Rustenburg ni mji ulio na utajiri wa madini ya platinum, jamii nyingi zinaishi kwa umaskini katika enoe hilo.

MSF linasema limegundua kuwa kuna haja ya kuongeza idadi ya maafisa walio na ujuzi wa kuchunguza ushahidi katika eneo hilo na idadi ya taasisi za kutoa huduma msingi za afya na huduma za kutoa ushauri nasaha kwa jamii.

Afrika kusini ni nchi ilio na visa vingi vya ubakaji duniani na kiwango kidogo cha watu kushtakiwa kwa makosa hayo.

Maafisa wa serikali wanasema kampeni za uhamasishaji zitahimiza waathiriwa wa ubakaji kutafuta usaidizi wa afya na pia usaidizi kisheria.

Tags