Kuendelea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1342-kuendelea_ukiukaji_mkubwa_wa_haki_za_binadamu_nchini_misri
Katika hali ambayo siku ya tarehe 11 ya mwezi huu wa Februari wananchi wa Misri waliadhimisha mwaka wa tano tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo dikteta Hosni Mubarak alipoondolewa madarakani, serikali ya Rais wa sasa Abdel Fattah el Sisi ingali inaendelea kukiuka haki za binadamu na hasa hasa dhidi ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2016 04:16 UTC
  • Kuendelea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Misri

Katika hali ambayo siku ya tarehe 11 ya mwezi huu wa Februari wananchi wa Misri waliadhimisha mwaka wa tano tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo dikteta Hosni Mubarak alipoondolewa madarakani, serikali ya Rais wa sasa Abdel Fattah el Sisi ingali inaendelea kukiuka haki za binadamu na hasa hasa dhidi ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin.

Meja Jenerali Amr al-A'asar, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Polisi alitangaza jana kuwa chuo hicho kimewafukuza wanachuo 40 kwa sababu ya kuwa na uhusiano na harakati ya Ikhwanul Muslimin.

Siku ya Jumatano, mahakama ya makosa ya jinai ya mkoa wa al-Mansura ilitoa hukumu kadhaa kwa wanachama 58 wa Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Sharif Futuh al-Qumash, mfanyabiashara wa mkoani al-Mansura wakati wa matukio yaliyojiri kwenye uwanja wa Raabiatul- adawiyyah. Mahakama hiyo ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa watu saba, watu watatu walipewa adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela na kazi ngumu, na watu wengine 21 walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.

Wakati huohuo siku ya Ijumaa iliyopita ya tarehe 12 Februari, maelfu ya madaktari nchini Misri waliandamana hadi mbele ya makao makuu ya jumuiya ya madaktari katika mji mkuu Cairo, kulalamikia kuachiliwa huru askari polisi tisa ambao waliwapiga na kuwajeruhi madaktari wawili wa hospitali ya al-Matariyyah iliyoko mashariki mwa Cairo. Hata hivyo polisi walikabiliana vikali na madaktari hao.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Misri wametangaza kuwa katika kipindi cha juma lililopita vjana 20 walitiwa nguvuni na askari polisi mjini Alexandria. Vijana hao walikamatwa kwa tuhuma za kupigana na askari polisi na kuichoma moto gari ya polisi ya mji huo. Vijana hao wana umri wa kati ya miaka 15 hadi 20, na kwa mujibu wa familia zao, idadi kadhaa miongoni mwao wameteswa na mmoja wao amepoteza kumbukumbu kabisa.

Gazeti la Los Angeles Times limeandika, sababu ya kuandamana madaktari nchini Misri ni utumiaji nguvu kupindukia na ukatili waliofanyiwa madaktari wawili wa hospitali ya al- Matariyyah na askari polisi tisa ambao ni kielelezo kimojawapo cha mwenendo usio wa kisheria na usio wa kibinadamu wa polisi ya Misri.

Kwa mujibu wa gazeti hilo linalochapishwa nchini Marekani, ripoti ya kamisheni ya haki za binadamu na uhuru wa maoni nchini Misri aidha inaonyesha kuwa zaidi ya watu 300 wametoweka katika kipindi cha miezi sita iliyopita; na hivi sasa kuna watu wasiopungua 16,000 kwenye jela za nchi hiyo.

Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Misri unaendelea kufanyika katika hali ambayo tarehe 11 mwezi huu wananchi waliadhimisha mwaka wa tano tangu dikteta Mubarak alipotimuliwa madarakani. Nukta muhimu ni kwamba moja ya sababu kuu za kufanyika mapinduzi ya Januari 25 mwaka 2011 nchini Misri ilikuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa na utawala wa Mubarak.

Lakini pamoja na hayo, serikali ya el-Sisi ambayo iliingia madarakani mwaka mmoja baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya Muhammad Morsi inaendelea kukiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko hata ulivyokuwa utawala wa dikteta Mubarak. Kupitishwa sheria kadhaa ikiwemo ya kuandamana na ya kupambana na ugaidi kumekuwa chachu ya kushtadi na kupamba moto ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Abdel Fattah el-Sisi.../